Bro Michu,

Naomba kutoa Waraka Wangu wa Shukrani kupitia Globu yetu hii ya Jamii. Leo 3/08/09 umetimia mwaka mmoja tangu nilipopata ajali mkoani Dodoma.

Sasa nimepona japo bado haujapona.Leo nimerejea Dodoma kuzuru eneo la ajali, ndipo nilipotulia na kutafakari, nikajikuta ninawiwa kushukuru kwa yote, ndio maana nimetoa waraka huu wa shukrani. Kwanza kabisa namshukuru Mungu, kuniruhusu kuendelea kuishi, kiukweli ni kama nilishakufa, Mungu Baba akanihurumia kunirudishia uhai ili niendelee kuishi.
Hii ni privilage tuu kwa sababu sikustahili. Nasema asante sana Mungu kuniweka hai. Pili naishukuru sana familia zangu za pande zote nikianzia kwa Familia ya Kasanga, Mayalla, Ukoo wa Kundi wa Kirua Vunjo Moshi, Ukoo wa Mmari wa Sanya Juu, Ukoo wa Mwingira wa Ndumbi Songea, mke wangu na watoto wangu wote 5 kwa yote waliyoyavumilia katika kipindi chote tangu ajali mpaka sasa. Asanteni Sana.
Namshukuru dereva wa Lori la Mafuta la Gapco aliyekuwa na ujasiri wa ajabu wa kuupekua mwili wa mtu aliyedhaniwa kufa, kutoa simu mfukoni na kupiga namba za mwisho zilizopelekea Timu ya PPR iliyokuwa Dodoma ikiongozwa na Adam, kunipatia msaada wa haraka mpaka hospitali ya mkoa wa Dodoma. Asanteni sana.
Nawashukuru madaktari na manesi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma tangu mganga mkuu, manesi wa zamu na daktari bingwa aliyelazimika kukatiza mapumziko yake ya jumapili na kuja kukesha usiku kucha na mimi hospitali mpaka nilipopata fahamu. Asanteni sana.
Nawashukuru sana wanahabari wenzangu waliokuweko Dodoma, ambao walisambaza taarifa zangu na hatimaye wateja wa PPR kwenye Maonyesho ya 88 na marafiki zangu wa Dodoma walikuja kwa haraka hospitalini sambamba na michango iliyowezesha kupata kila huduma iliyohitajika mpaka nilipohamishiwa Moi, Asanteni Sana.
Navishukuru vyombo vya habari na jumuiya ya wanablog mbalimbali kwa kuutangazia ulimwengu kuhusu ajali yangu kulikopelekea ndugu jamaa na marafiki waliotapakaa dunia nzima kupata taarifa, hivyo waliniombea uponyaji wa haraka na weghine kutoa support ya hali na mali.
Namshukuru Mdogo wangu Isaack Kassanga kwa kukubali kugharimia ndege ya kukodisha kuniairlift toka Dodoma mpaka Dar baada ya taarifa ya awali kuwa nimevunjika spinal, pia namshukuru dereva wake aliyekuja Dodoma na strecher vehicle kunifuata na support team. Asanteni Sana.
Nawashukuru sana Madaktari na manesi wa kitengo cha mifupa MOI wakiongozwa na Dr. Kahamba na Daktari wangu Dr. Marealle kwa jinsi walivyohangaika na mimi kwa mwezi mzima niliolazwa hapo Moi mpaka kupata nafuu na kuruhusiwa na kusubiri matibabu zaidi nje ya nchi. Asanteni sana.
Nawashukuru Ndugu, Jamaa,marafiki na majirani waliokuja kunitembelea pale Moi kwa michango yao na zawadi mbalimbali. Sikuwahi kulazwa hospitalini maishani mwangu, na sikuwa na utamaduni wa kutembelea wagonjwa mahospitalini, mpaka niliposhuhudia jinsi nilivyotembelewa nikagundua thamani ya kuwafariji wagonjwa na kuthibitisha ni kiasi gani unathaminiwa. Asanteni Sana.
Pia nawashukuru wale wate ambao hatakufahamiana kabla, sio ndugu, sio jamaa na wala sio marafiki, ni watu tuu wa kawaida lakini waliguswa wakaja hospitalini kunijulia hali na kunifariji, wengine wakija kuangalia wagonjwa wao lakini na mimi nikawa sehemu ya ndugu zao. Asanteni Sana.
Nawashukuru wanahabari waliokuja kunifariji muhimbili akiwemo Athumani Hamisi wa Daily News na Habari Leo ambaye naye kwa bahati mbaya pia alipatwa na ajali mbaya ya gari bado angaliko Afrika Kusini na Heri Makange wa Channel Ten (RIP) ambaye tulizungumzia pikipiki, nikiwa hospitalini nchini India nikapata taarifa ya kifo chake kwa ajali ya Pikipiki. Mungu ampatie Athumani Hamisi uponaji wa haraka na amrehemu Heri Mkange apumzike kwa amani.
Kitendo cha mimi niliyekuwa kitandani sasa nimesimama Athumani bado hospitalini na Heri katangulia mbele ya haki, najiona bado mimi ni mwenye bahati sana. Asanteni sana.
Nawashukuru viongozi mbalimbali wa dini, wa kiroho, vikundi vya wanamaombi, wachungaji wa wokovu, walokole na watu wa Jumuiya yangu ya Mtakatifu Gabrieli, Mbezi Beach kwa kuja na kuniendeshea maombi mbalimbali. Asanteni Sana.
Nawashukuru sana majirani,ndugu, jamaa na marafiki wote wa Tanzania, Marekani, Canada na UK kwa kuitikia mwito wa mchango kugharimia sehemu ya gharama za Matibabu zaidi nchini India na nchini Afrika Kusini na kuniwezesha kufikia hapa nilipofikia. Asanteni Sana.
Nawashukuru wateja wa PPR kwa kunivumilia, kwani walishalipia matangazo ya 88, kufuatia ajali hiyo, matangazo yao yaliathirika, huku fedha zao zimekwenda bila kunidai au kutakiwa kurudisha on the spot. na wengine tulishaandikishana mikataba ya malipo na bado wakaendelea kulipa bila huduma za papo kwa papo. Asanteni Sana.
Navishukuru vituo vya Redio na Televisheni, vikiongozwa na TBC, ITV, Star TV na Channel Ten kwa kurusha program za PPR kabla ya ajali yangu zikitarajia kulipwa lakini zikalazimika kukaa mwaka mzima bila kulipwa na mpaka sasa vingine bado havijalipwa. Samahani sana kwa usumbufu uliojitokeza na Asanteni sana.
Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya, Madakitari wa kitengo cha rufaa za nje pale wizarani nchi kwa kuniwezesha kwenda hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu zaidi na kugharimia matibabu ya msingi. Asanteni Sana.
Namshukuru Balozi wa Tanzania nchini India, Balozi Eng. John Kijazi na timu yake yote ya ubalozini na familia zao wakiongozwa na kaka yangu Seneta Makongoro na Yahya kwa kugeuka ndio ndugu, jamaa na marafiki wa wagonjwa watanzania wote wanaolazwa nchini India, hadi kujikuta namna ya kusherekea sikukuu kama Krismasi na Mwaka mpya ni kuwatembelea wagonjwa ambao ki ukweli sio ndugu zao kinasaba bali tumekuwa ndugu Kiutanzania. Asanteni Sana.
Nawashukuru wagonjwa wenzangu ambao tulilazwa wote Appolo Hospital, wenye nafuu kidogo tulitembeleana kufarijiana, huku waangalizi wao wakiwa ndio ndugu wa wote kwa kusaidia kuhudumia bila kujali nani ni nani ikiwemo juhudi za akinamama waangalizi kupika vyakula vya Kitanzania mara kwa mara wakishirikiana na wake za maofisa ubalozini na kutufanya waTanzania kujisikia tuko nyumbani, Asanteni Sana.
Nawashukuru madaktari wangu wa Apollo wakiongozwa na Dr. Prasaad na Dr. Karbinder, manesi, kwa huduma zao za kitabibu na vifaa vya kisasa vinavyoniacha na maswali bila majibu hivi ni kweli Tanzania hatuwezi?!. Nawashukuru sana.
Pia nawashukuru wahudumu wasio wa tiba wakiitwa Bayer kwa kutoa huduma nyinginezo kama hotelini na mgonjwa kunyenyekewa kama mfalme, kitu ambacho katika hospitali zetu, bado. Nawashukuru sana.
Nawashukuru viongozi na Watanzania waliotembelea India kwa ziara za kikazi, kutembelea wagojwa na kuwafariji hufanywa ni sehemu ya ziara zao.Hebu fikiria wewe ni mwananchi tuu wa kawaida umelazwa hospitalini ughaibuni, huna ndugu, unakuja kutembelewa mara na mawaziri, mara wakurugenzi, mara balozi, japo unaumwa, lakini unapata faraja fulani kwa kumbe na wewe ni mtu muhimu!..Asanteni Sana.
Nilipata ajali nikikabiliwa na deni fulani Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo nilijaribu kula nondozzz ya LL.B. Nawashukuru sana wanafunzi wenzangu, wafanyakazi na walimu in particular Dean Prof. Mchome, Prof. Kabudi na mwalimu kijana Kitta, kuniwezesha kulilipa hilo deni nikiwa kitandani tangu Muhimbili. Sasa mimi ni mwandishi wa habari, mtangazaji na mtayarishaji wa vipindi vya televisheni huku nikiwa nimeshalamba nondozzz langu la LL.B ya UDSM tena siyo PASS!. Thanks to them. Asanteni Sana.
Sasa ni mwaka mmoja umepita tangu ajali hiyo ilipotokea. Mimi nimerejea rasmi nyumbani, nimepona japo mkono mmoja bado. Kinachoendelea ni kukusanya tena nguvu, kurejea nchini India kwa matibabu ya mwisho. Hivyo ndugu zangu, jamaa na marafiki, msishangae nitakapo wapigia hodi hodi mara muda muafaka ukiwadia.Natanguliza shukrani. Asanteni Sana.
Kutokana na mkono mmoja bado haujapona, ni bahati mbaya sana siwezi tena kushika camera, wala kazi za kuchakarika na mahangaiko ya upiganaji kama zamani. Hivyo kwa sasa, nimelazimika kujishikiza mahali nikifanya kazi za kiofisi.Namshukuru sana mwajiri wangu wa sasa kwa kunikubali hivi nilivyo. Naishukuru timu mzima ya PPR ikiongozwa na Adam na Muddy, ofisi ya PPR Mkwepu, WDC Mkwepu na vijana wote wa Mkwepu kwa kunilinda na kuhakikisha kazi za PPR zikifana kawa kawaida.Hata hivyo, bado ninafanya part-time PPR siku za Jumamosi na Jumapili. Hivyo nawashukuru sana wateja wa PPR ambao bado wamesimama na mimi katika hali nilio nayo na wanaendelea kunitumia. Asanteni Sana.
Nawashukuru na watu wengine wote wenye mapenzi mema, nawashukuru wale ambao walitaka kuniona hawakujua wanione wapi. Nawashukuru hata wale tunaokutana mara kwa mara wengine wakishtuka kuniona hivi nilivyo, wengine kwa kutoamini macho yao na wengine hata wakitokwa machozi. Asanteni Sana.
Namalizia kwa kuwaomba mzidi kuniombea nipate uponaji wa kamili, cha muhimu ni mimi nimeikubali hii hali nilionayo kwa sasa kuwa hivi nilivyo ndio sasa niko hivi, at the same time, nothing is imposible under the sun hivyo bado nina matumaini ya uponaji zaidi.
Ni vigumu kumshukuru kila mmoja wenu ambaye ajali yangu imemgusa kwa namna moja au nyingine. Natamani sana kuataja wote, sitaweza kuwamaliza ila nawashukuru sana Wote nasema ASANTENI SANA.
Pascal Mayalla
+255 784 270403

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 24 mpaka sasa

  1. ndugu pasko yote uliyoyasema yanamsingi sana.mimi kama mtanzania mwenzako nakupa pole kwa yote yaliyokukuta yote hayo sisi wakristo tunaamini ni mipango ya mwovu shetani lakini kwa nguvu za MUNGU shetani aliaibika siku ile ile uliyopata ajali ndo maana hukufa.pili niipongeze familia yako kwa moyo wa uvumilivu ktk kipindi ulichokuwa matibabuni kwa namna moja au nyigine waliteseka kifikra kuwa baba yetu ni mgonjwa,mume wangu ni mgonjwa BASI NINAUNGANA NAWE KUMSHUKURU MUNGU PEKEE

    ReplyDelete
  2. Pole kaka, Pasco
    Mungu atakuongoza zaidi.

    ReplyDelete
  3. Pole sana kaka Pascal mh nimesoma maandishi yako kwa kweli machozi yamenitoka...Mungu Atakusaidia utapona kabisa .....Fanya mazoezi u will be better.

    ReplyDelete
  4. Du! Mwanangu ujumbe umenigusa ni mzito, Mwamini Mungu hakuna linaloshindikana kwake yeye hufanya njia pasipo na njia; kama bado upo hai kutokana na ajali ile basi anamakusudi makubwa nawe; amini na omba akuzidishie IMANI na utarudia hali yako ya mwanzo ukiamini.

    ReplyDelete
  5. PAMOJA NA POLE NYINGI LAKINI NASIKITIKA KUMWAMBIA BWANA MDOGO MAYALA AACHANE NA PIKIPIKI KAMA SIKOSEI HII NI MARA YA PILI SASA KUPATA AJALI TENA ,KUMBUKA MARA YA TATU HUENDA MUNGU ASIWE WAKO ACHANA NA KUENDESHA PIKIPIKI KABISA HUU NI USHAURI WANGU BINAFSI,MAANA TANZANIA NAJUA ASILIMIA ZA KUPATA AJALI KWENYE PIKIPIKI NI KUBWA KULIKO GARI

    ReplyDelete
  6. Mr. Pasco nilikujua kupitia kile kipindi maarufu sana kilichokua kikiitwa "kitimoto" hakika nilikua najitahidi kutokikosa kipindi kile. Pole sana but thank God you are Pascal Mayalla bro.

    ReplyDelete
  7. Pascal kaka yangu pole sana,maneno yako uliyoandika yamenigusa sana,na umenifanya nikumbuke mbali sana enzi hizo tuko Tabora unakumbuka mjomba Mayalla(RIP) alivyokua akizipenda pikipiki enzi hizo YAMAHA!mpaka watu wakawa wanamuita mzee YAMAHA, wewe nae umerithi nakushauri hizo pikipiki achana nazo kabisa,tena ziogope.Tutawasiliana zaidi.

    ReplyDelete
  8. POLE SANA PASCAL!

    Mungu ni wa ajabu sana na panapotajwa jina lake kwa imani uzima na uponyaji unapatikana.Ushauri wangu tu ni uendelee kumtegemea sana Mungu kwani yeye pekee ndiye amekuepusha na dhahma iliyokuwa mbele yako.NA ASHUKURIWE YEYE PEKEE KWA SABABU ANA UWEZA.

    Amen.

    Mdau,Oxford.

    ReplyDelete
  9. mr.pasco pole sana .do u know what/ kaka wewe ni mtu wa watu ujisikii uchague mtu wa kuongea nae nimeshawai kufanya kazi na wewe ulitusaidia sana kwenye maswala ya kulipwa.ni maombi ya watu unavyo msaidia mtu yeye anakuombia kwa mungu. mungu yu mwema kaka atakusaidia na mpaka sasa amekusaidia utakuwa kama mwanzo.tupo pamoja katika maombi ubalikiwe kaka.

    ReplyDelete
  10. MICHUZI SISI,wengine ni wabeba box,so time is mine,ikiwezekana jaribu ku edit hatuna muda wa kusoma magazeti

    ReplyDelete
  11. Kaka Pascal nimesoma ujumbe wako mwanzo hadi mwisho lakini ktkt ilinibidi nitafute leso nianze kufuta machozi. Kweli MUNGU ni wa ajabu na nasema MWACHENI MUNGU AITWE MUNGU kwani ni mengi mema na magumu ya ajabu anatufanyia LKN sisi bahati mbaya mioyo ya kiibilisi imetuganda kiasi cha kushindwa kumrudishia mungu shukrani. Pascal kama ulikuwa huamini kama MUNGU yupo, nafikiri hii ajali imekuhabarisha zaidi kuhusu uwepo wa mungu. Tuzidi kumshukuru na kumwomba mungu ila isiwe ni wakati wa shida tu ila hata wakati tukiwa matawi ya juu mungu apewe sifa pia. Pascal pole sana na mungu akutangulie katika uponyanyaji wako.

    Kuhusu kifaa cha moto ulichokuwa unatumia wakati wa ajali, mimi nafikiri ajali ni ajali tu haijalishi ni baiskeli, pikipiki, gari, treni au ndege. Wakati wako ukifika utaondoka tu hata wakati mwingine inaweza kuwa ni kwa ugonjwa wa kawaida tu. Cha msingi ni kuwa makini katika yale ambayo tunaweza kuyaepuka kama kipindupindu, UKIMWI, ULEVI ETC.Linapotokea suala la safari, mara nyingi huwezi kumkataza mtu kutumia chombo fulani na hicho chombo pia kinakuwa hakina guarantee ya usalama.Hebu fikiria kwenda marekani toka Dar kwa baiskeli au kwenda Mbagala toka posta Dar kwa ndege. Hilo haliwezekani kwa hiyo lazima aina fulani ya usafiri itumike na sala juu

    ReplyDelete
  12. RUDIA TENA.....MANA WEWE HUO NI MCHEZO WAKO.......

    ReplyDelete
  13. Pole sana kaka Pascal. Umenikumbusha mengi ambayo sisi binadamu tukuwa na afya tunayasahau. Hasa hili la kutembelea wagonjwa na kuwajali wenye mahitaji mbalimbali.

    Baada ya pole, narudi kwa huyu mpumbavu anon wa Aug 03 01:35pm. Umenichefua sana. Ndio maana mnaitwa waosha vinywa! Kama unaona huna muda si uache kusoma? Unaleta ujinga hata kwa mambo ya maana.

    ReplyDelete
  14. niliumia sana nilivyokuona siku moja pale uk embassy mkono wako uliokua ukishika mic jinsi ulivyo kwa sasa, roho iliniuma sana jinsi ambavyo haukua na ballance mpaka ubebe na mkono mwingine,kwa kweli hujafa hujaumbika, muda ukifika tujulishe kwenye blog ,tuko pamoja kwa maumivu haya
    pole sana

    ReplyDelete
  15. paschal mara nyingi umeambiwa usiendeshe piki piki bila HELMET.
    UMEKUWA MKAIDI NA HUSIKII.
    SASA UMEWATIA HASARA WATU WANGAPI KWA UZEMBE WAKO?
    UZURI ULIAMBIWA MAPEMA HUKUSIKIA.ENDELEA MAANA MKAIDI HAFAIDI HADI SIKU YA IDDI.

    ReplyDelete
  16. Mzee mwenzangu Pascal uache sasa mambo ya kipuuzi kusafiri/endesha pikipiki. Watoto watano bila baba ni noma. Na kilio chako hapa ni cha abunuwasi kuanguka kwa kukalia tawi alilokuwa anakata. Lakini pia nakutakia afya njema upone haraka. Pyhsical therapy ni muhimu.

    ReplyDelete
  17. Pole sana kaka Mayalla,machungu yako na Mungu anayajua.Tuzidi kumwomba-Kwa Mungu yote yanawezekana.Mdau wako wa Kyela -Mbeya

    ReplyDelete
  18. Kwanza Pascal nakupa pole na tunashukuru kwa Shukurani zako, na kuelewa ya Kwamba Mungu yupo na ndio Muokozi wako. Kwa wale walisema avae helmet au ache mchezo wa kipuuzi naona hapa si mahali pake, kwani kama kujutia kosa lake ameisha fanya hivyo, na pia ajali yake haikutokana na kuto vaa helmet, maana ameumia Mkono, na toka amepata ajali kwa kuwa mkono moja bado hauna nguvu za kutosha ni wazi hawezi kuendesha pikipiki ( Tuku Tuku?) na Pia unaweza kumwambia mtu asifanye kitu kwa lugha ya kistaarabu.
    Ila kama una matatizo nae mengine hiyo ni nje ya hapa.

    ReplyDelete
  19. Brother Pascal,kila mwenye subira basi yu pamoja na mwenyezi Mungu.Sisi nduguzo tunakuombea,nawe pia endelea kuamini MUNGU kwamba utapona,naye atakuponya Inshaalah!

    Nduguyo-Mkulima kijijini Gezaulole.

    ReplyDelete
  20. Pascal,

    Taarifa yako kwa kweli imewagusa binadamu wote waliozaliwa na mwanamke mwenye huruma. Muumba Mungu amekuwezesha kupona hadi hapo ulipo natumaini tuendelee kuwa na matumaini kwani Muumba wetu hamtupi mtu. Mungu akuongezee baraka na neema tele. Nazidi kukuombea neema na nguvu na afya tele Pascal

    ReplyDelete
  21. yes bro mayal, pole sana kwa ajali na tunakutakia uponaji mwema,tutaendelea na sara zetu na punde si punde utarejea shughuli zako kama zamani, na mwisho hongera kwa nondo hiyo
    wadau,michigan,usa.

    ReplyDelete
  22. MIMI NA OMBI TUSHIRIKIANE TURUDISHE KITI MOTO CHETU. .NAONA TANGU DUNI HAJI ATEME CHECHE KIKAISHIA MITINI HIVI HIVI. SASA HIVI NDIO ZAMA ZA UWAZI NA UKWELI HALISI, WAKATI ULE ZILIKUWA KAULI NAZARIA ZILIZO JAWA NA MAMBO YA KUKANUSHWA KWA HABARI ILIZOKANUSHWA( NEGATING OF NEGATIONS)
    MORIS CLASSEMATE HAPA

    ReplyDelete
  23. JAMANI KAMA YAMESHATOKEA NI BASI TUSAFISHE VINYWA VYETU HUU SIO WAKATI WA KUTOLEANA LAWAMA ILA KUFARIJIANA. NAOMBA WOTE WALIOTOA LUGHA ZA LAWAMA WAACHE SIYO TABIA NJEMA NA KUMBUKA HUJAFA HUJAUMBIKA HUJUI NI YEPI YANAWEZA KUKUFIKA PIA WEWE TENA KWA UZEMBE USIOTARAJIWA.NASEMA JAMANI TUOSHE VINYWA

    ReplyDelete
  24. Enter your comment...nakukubali sana pasco leo yapata miaka nane tangu upate ajali, vipi ulishaacha kuendesha pikipiki? moses samwel ryoba ppftower.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...