Ndugu Michuzi,

Naomba uniwekee hii ili nipunguze machungu..Nimechoka kusoma mada za watu zinazosema lini walio nje ya nchi watarudi nyumbani. Miaka mingi imepita toka nianze safari ndefu ya kutafuta elimu..safari hii ilianza 1986 shule ya msingi Kawe. Nia na madhumuni ya safari hiyo ni kujikomboa katika umasikini kwani kwangu mimi elimu ndie mkombozi pekee. Nikikumbuka hali niliyokuwa nayo nyumbani ilinisukuma kusoma sana ili niweze kutatua matatizo yaliyokuwa yanasumbua jamii nzima.

Baada ya kumaliza form six pale Tambaza, nilibahatika kupata nafasi ya kwenda nje (si kwa kupelekwa na serikali) na nikatia nia kuwa nitaitumia nafasi hii kusoma. Nashukuru kua Mwenyezi Mungu alinifanyia wepesi katika nia hiyo kwani tujuavyo ukikumbuka umasikini uliotoka nao nyumbani jawabu rahisi ni kubeba boksi. Mimi nilibeba boksi usiku na mchana nikaenda shule. Sikuwa na jumamosi wala jumapili siku zote nilikuwa niko kwenye mihangaiko ya kubeba boksi na kubeba vitabu.

Nilitaka kuwa Medical Doctor kutokana na Malaria yaliyokuwa yakinisumbua kila baada ya miezi sita nilipokuwa nyumbani.  Lakini nilipoona computer nikavutiwa na uwezo wake nikaamua kusoma Diploma ya Computer Programming (IT) kwasababu nilijua naweza kuwezesha madaktari kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi kwa kutoa tiba za uhakika. Nilivutiwa sana na mfumo wa hospitali utumiwao hapa UK. Nikafanya kuwa lengo langu kutengeza mfumo mzuri zaidi ya huo kwa kuwezesha hospitali nzima kujiendesha kwa ufanisi zaidi kwa kuangalia jinsi taarifa zinavyosafiri toka mgonjwa anapofika hospitali mpaka anapopatiwa tiba na kutoka hospitalini.

Nilifaulu vyema nikapata nafasi ya kujiunga na Chuo kikuu ambako huko nikapata nafasi ya kutengeneza mfumo huo. Kwa muda wa miaka mitatu nili design na kutengeneza mfumo huo kiasi wanafunzi kutoka kwenye nyengine za Afrika walivutiwa sana hata wakanishawishi niwauzie ili wakautumie kwenye nchi zao. Mwanafunzi mmoja toka Sudani aliniomba na nikamkubalia kutumia mfumo wangu kwa ajili ya project ya mwisho ya Master degree yake na akapata First Class kutokana na ubora wa mfumo huo. Hii ikanipa moyo kuwa nikimaliza na nikirudi nyumbani basi nchi yote tutafaidika na mfumo huo.
Mwaka 2007, nikapata nafasi ya kwenda nyumbani baada ya kumaliza Degree yangu ya Mwanzo ya Bachelor of Electronics and Computer Engineering. Nikanunua projector, nikatengeza powepoint presentation slides kwa ajili ya kuja kuonyesha mfumo huo nikiamini utaleta mabadiliko chanya katika utoaji huduma za afya kwenye nchi nzima. Ndani ya ndege nilipata shauku kubwa ya kufika haraka ili niweze kuanza kuokoa maisha ya watu kwa kuwezesha madaktari kutoa huduma bora ya uhakika. Nilishafanya mawasiliano na watu wajuu mmoja wapo akiwa waziri wa afya kipindi hicho alikuwa na taarifa yangu, yeye akanielekeza kuonana na mkurugenzi wa wizara ya afya kipindi hicho.

Nilipofika sikujali machofu ya safari kesho yake nikatinga ofisini huko baada ya kusota masaa zaidi ya manne nikaambiwa nije kesho. Kesho yake asubuhi mapema nikawa nimefika , baada ya masaa mawili ya kusubiria kwenye benchi nikapata nafasi ya kuonana na Mkurugenzi. Huko ndani baada ya kujitambulisha nilipotamka neno computer tu mkurugenzi akaniambia nikaonane director wa IT nilipoulizia ofisini kwake nikaambiwa yuko likizo miezi mitatu. Niliporudi ofisini kwa mkurugenzi nikaambiwa nikaonane na vijana wa IT pale chini. Nilipokwenda hapo kwenye ofisi ya IT, nikakuta vijana watatu wakipiga soga na computer moja iliyokuwa mezani ikanivunja moyo.
Kwa bahati nillikutana na Daktari mmoja toka Arusha anaitwa Doctor Chamba, aliniuliza ninasubiri nini pale ofisini nilipomweleza akafurahia na akataka kujua zaidi lakini alikuwa safarini kwenda India. Nikarudi nyumbani kichwa chini..Jambo lililouma zaidi nikwamba sikupata hata kuonyesha hizo slides. Nakumbuka Mama yangu alinambia labda nirudi baada ya miaka hamsini watanielewa.
Nikakwea pipa kurudi nilikotoka maana nimekuwa mgeni nyumbani kwangu. Mwaka 2008, wazungu wakaanza kuja Afrika kuleta mifumo ambayo haifikii hata robo ya huu niliounda mimi na wakapokewa kwa mikono miwili nikabaki natazama kwa google kuona nini kinaendelea. Jambo la kusikitika mifumo ya majaribio waliyokuja nayo imekuwa mitego kwa taifa kwani habari zinahifadhiwa ulaya mgonjwa yuko Afrika. Hawahitaji kufanya uchunguzi kujua kama ni taifa la wazima ama wagonjwa kwani taarifa zinafika kwao wakazichambua wanavyotaka wao. Taarifa za afya ni nyeti leo hii majaribio yao yamewezesha kuzifanya rahisi kwa wao kuzipata.

Niliporudi nikapata nafasi ya kusoma Masters of Nanotechnology, na baada ya kufaulu vyema nikapata Scholarship ya kusoma PhD (toka kwenye kampuni iitwayo Oclaro inayojishughulisha na mitambo ya mawasiliano ya Fiber) katika masuala ya quantum physics. Nashukuru Mola kuwa nimefaulu mtihani wangu wa PhD mwezi wa tano na sasa nimekuwa Doctor.

Nilipojaribu kutazama kilichoendelea katika mfumo wa Afya naona bado ule mfumo niliouacha miaka mitano nyuma una nafasi ya kuboresha na kubadili utoaji huduma za afya si kwa Tanzania tu bali kwa nchi nyingi za kiafrika.  Nataka kurudi tena Tanzania mwezi ujao lakini sijui ni vipi nitapokewa.

Nakuja nikiwa ninashauku mpya kuwa nitatimiza lengo langu la kuboresha utoaji huduma za afya kwa watanzania ili tusonge mbele kimaendeleo kwani mgonjwa hafanyi kazi. Afya ndio chachu ya maendeleo ya nchi zote zilizoendelea.

Mdau Dr. Sayid Ally Sayid

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 33 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 28, 2012

    Kwanza pole sana kwa yaliyokukuta. Hiyo ndiyo Tanzania. Cha kushangaza ni kwamba ulikulia bongo lakini ukasahau hulka za watu wa nchi yako. Wabongo wana wivu, choyo na roho mbaya, japokuwa sio wote. Wanapopata mahali pa kufanyia kazi wanajenga uzio kuzuia changamoto zinazojitokeza na kusahau kwamba wanatakiwa wakubaliane na changamoto zinazokuja kwani penye changamoto ndipo penye mafanikio. Wakisikia una utaalamu kama huo wenye vyeo vya hiyo taaluma huanza kuogopa kwamba utawachuulia kazi zao. Wengine hawahofii kupoteza kazi bali huhofia kufunikwa. Na wengine watakuwa wameshajitengenezea mitego ya wizi kwa kutumia taaluma hiyo. Hivyo unapokuja wewe utaoneka "threat".

    Hivyo basi kabla ya kuja Tz ulipaswa ujiandae kwa lolote ambalo lingetokea.

    Pili naomba nikupongeze kwa kuwa na uzalendo. Watu kama wewe ndo mnatakiwa ili taifa lisonge mbele kisayansi na technolojia. Kwa hiyo usife moyo katika kutekeleza uzalendo wako huo. Usihesabu makosa yaliyopita jaribu tena.

    Ushauri wangu tu ni kwamba uisiweke pesa mbele sana kwani ukifanya hivyo kila mtu atakukimbia. Jijenge kwanza, jenga heshima yako kazini, onesha umaarufu wako kivitendo epuka kujikweza na mwisho pesa zitakuja zenyewe. Bongo pesa ipo hasa unapokuwa na kipaji ambacho ni nyeti na watu wengi hawana.

    Mwisho maisha ni popote. najua huko uliko unaweza kupata pesa nyingi sana lakini umeamua kurudi home. Hata hivyo ukiona hawaelekei rudi zako mamtoni kaandike kitabu uwatumie watanzania. Kitakuwa fundisho kwa wengine wanaokuja. Tuko katika kipindi kigumu ambacho mindset za watanzania walio wengi si nzuri na zinahitaji ukombozi kabla hatujaanza kikimbizana na maendeleo.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 28, 2012

    Jaribu tena usikate tamaa ,inawezekana waliopo sasa watakuelewa.Ikishindikana nenda kauwauzie idea jirani zetu kwa mh.Kagame halafu wale wakifanikiwa sisi tutakuwa na mpango mkakati pamoja na safari ya mafunzo tukajifunze kwao hatimaye mfumo huo utafika hapa kwetu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 28, 2012

    Omba appointment uonane na JK kwa jinsi alivo na shauku ya kuwatafutia maendeleo wananchi wake kila kona ya dunia atafurahi kuona mtanzania amejitokeza kukidhi kiu yake. Mungu Ibariki TZ

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 28, 2012

    Pole sana ndugu yangu haiyo nmdio inaitwa bongoland.Mimi nakushauri kuwa usiwe unapata tabu wakati wewe ndio unayo hiyo project yako nenda nchi nyingine za afrika kauze hiyo project upate pesa na uangalie ustarabu mwingine.Nasema hivi kwa sababau mimi yalimkuta ndugu yangu alikuwa na software moja akaingia kenye tenda hapo nyumbani.Kulikuwepo watu wengi lakini yeye peke yake ndiye alikuwa na sample pamoja na slide ya kuwaonyesha watoa tenda,cha ajabu alishindwa tenda kw akuambia kuwa yeye hakuapata kwa sababu anaishi ulaya na aliyeshinda alipewa muhindi anayeishi nyumbani ambaye siyo raia. basi akawa anafany ampango wa kurudi majuu cha ajubu wale watoa tenda walimpigia simu na kumwambia kuwa yule muhindi anataka kuongea naye na wakampa contact zake, walipoonga muhindi akamwambi jamaa amuuzie software yake ili yeye akawauzie jamaa lakini apewe hati miliki. ndugu yangu alikataa na hiyo software anayo mpaka ssa aliwauzia nchi ya jirani.Pia mfano mwingine kuna doctor mmoja bingwa wa upasuaji wa moyo mtanzania mwenzetu aliamua kuja na machine ya ugonjwa huo nyumbani ili iweze kuwasaidia watu.kwanza aliongea na wizara kila kitu kabla hajaja wakamwambia hakuna shida wewe njoo utapata kibali na kila kitu.Alipofika ilikuwa ni kuzungushwa hapa na pale hakuna kibali wala ushirikiano toka wizara hadi madaktari bingwa wa muhimbili alikuwa anapingwa chenga za ajabu. ukiangalia machine ameshazitoa bandarini kaziweka nyumbani kwake hawezi kufany nazo chochote na ilimgharimu pesa nyingi sana na mwishowe alipatwa na majonzi mengi na mwenyezi mungu alimchukuwa.Kwa hiyo wewe kama unarudi usiwe na high expectation ya kupata ushirikiano na pengine hata kumuona kiongozi yoyote chukulia kama unakwenda kuonanan na wanyama.Ishallah mungu akusaidie kwa safari yako.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 28, 2012

    Unajua tatizo la Tanzania ni corruption ndugu yangu, tofauti na uingeleza kila mtu anapenda maendeleo. Mfano mkurugenzi anasahau kwamba kwa kuwa wa kwanza kuprovide hiyo technology inaipa sifa hospitali na hivyo ingeweza hata kuongezewa mshahara wake kazini, pia wana research wengine wangekuja kwake kutaka feedback kuhusu hiyo system anayoitumia. Hatuna moyo wa maendeleo na pia tunamwona mzungu ndie atakayeleta maendeleo bila kujua kwamba nayr pia anatuibia. Hizi ndizo sababu zinazofanya watanzania wengi wenye vipaji kutorudi nyumbani na kubaki huko walipo.

    Mume wangu naye ni softaware developer, alijaribu kwenda nyumbani na hiyo softaware ya hospital lakini njoo kesho nazo zilikuwa nyingi, alioffer even bure wajaribu waone kama ipo vipi, lakini hakuna aliyetaka hata kuitest. Yaani inakatisha tamaa kwa kweli. Mwaka jana nilienda Tanzania nikaona kuna groups za watu ambao ni developers huwa wanapata deals toka mahospital mbalimbali wakaniambia ni vizuri uwepo palepale then baada ya miezi ya kusuffer utakuja fanikiwa.

    Hivyo usikate tamaa jibane hivyohivyo utafanikiwa.

    Mama H

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 28, 2012

    Nadhani watu wamekupa mawazo mazuri, muhtasari wake ni kama hivi:
    1. JK ni mpenda maendeleo na anapingana na mdau aliyeleta mada ya kuwa watanzania rudi nyumbani. Yeye alipokuwa ziarani msumbiji na itali aliwaasa wabongo kuwa mkipata nafasi wavute wenzenu waje. kwa maana ama ulaya au bongo usimuite mtu njoo kwa kuwa wewe una duka au kazi nzuri, muite kama anaweza kufungua duka au akapata kazi nzuri, iwepo. hayo nido maendeleo nandiyo kutafuta. ina maana, walio tanzania sio wote watanzania, wapo wazungu, wakenya na umesikia wa-ethiopia wanakuja na wengine wamekufa dodoma. ni kutafuta duniani kote. na hapo tanzania, unaweza kwenda Mwanza maisha yakakushika, lakini mtu akakwambia kuna kazi arusha ukaenda ukafanikiwa. uisende mwanza au arusha kwa kuwa kuna mtu tajiri, na wewe ukategemea utakuwa tajiri, kwa sababu tu uko sehemu ile.
    2. JK pia anapenda wabongo wenye vipaji warudi bongo kama kuna kazi za kufanya au mchango..mfano unamkumbuka gavana wa benki..pamoja kwamba alichemsha baada, lakini kazi aliifanya. kuna website ya ikulu, muandikie barua pepe, nasikia Mkapa alikuwa anasoma emails zake na balozi Maajar wa UK an USA..naamini na JK anasoma, kwani binafsi naona ana upeo kuliko wana siasa wengi..mfano anaruhusu watu hata wamkashifu kwa jina la uhuru wa mawazo..kama uganda utaburuzwa. kwa hiyo,
    usirudi ukiwa na high hopes, watu wamekupa vigezo kwani jamaa wanaweza kukukandamiza.
    lakini kwa kuwa una elimu yako, utafanikiwa kokote duniani.
    3. mdaua aliyesema rudi Bongo, naona kweli ana hisia za kimaskini, kwa kama wewe umerudi ukapata kazi ya ukurugenzi, haimanisha kila mtu akirudi atapata kazi hiyo, maana wewe umeshapta. na ulaya kumuonaamevaa kandambili haimanisha anashida, ni uamuzi..utajiri wa bongo kama Busha, unauona kwa mbebaji, hapa sio hivyo na kwa maneno mengine walifanikiwa kwa kurudi nyumbani ni ama walikuwa wana pesa ya kuwekeza waliyoata kwa boksi au elimu ya kupata kazi nzuri na kuendelea. mfano Masha katoka USA kaja akafanikiwa, ana masters, January Makamba alipiga boksi wakati anasoma, lakini kwa sabau ya elimu yake karudi sasa mambo mswano., nk. Haya Mwamoo Hamza na Phd, kasoma USA na anafanya kazi lakini wakati anasoma alipiga boksi kama kazi.
    hitimisho ni kuwa mtu utaenda kokote maisha yanakokutuma mama kutafuta elimu, deal(biashara) au kazi. wapo waliamia Morogoro kwa sababu mambo kule safi, na wale walioko Dar kwa sababui na jiji, lakini maisha taabu..afuatilia wapi kuan deal ama kikazi au bishara na amia uko, kama ni Ulaya sawa, Nariobi, DRC US nk

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 28, 2012

    mimi ni kijana wa kitanzania ninae penda nchi yangu sana hasa kimaendeleo, nimesomea software engineering na computer security,kwa anaye weza kujua jinsi gani ya kumwona rahisi tusaidieni, nina mawazo mazuri sana ya nchi yangu na tatizo ni kama alilosema mchangiaji wa hapo juu, labda rais wetu pekee ndie mwenye kupenda nchi yake iwe na maendeleo wengine kula wao tu

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 28, 2012

    Mdau hivi unacho wanachokiita intellectual property rights? nadhani ungefanya hima kwanza kuisajili hiyo program uliyounda na halafu ndio jitihada zingine ziendeelee, mimi naungana na wale walioshauri kwamba ikiwezakana tembelea kwa Kagame akajaribu halafu habari zitatuifkia hapa kwetu bongp na hivyo kuiweza kuichukua na kuingiza katika mfumo wetu.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 28, 2012

    MIMI SINA LA KUCOMMENT HAPA,,WADAU HAPO JUU WAMESEMA KILA KITU!,,,NINACHOCHANGIA NI WEWE TU UWEZE KUONANA NA RAIS,KAMA HAKUNA JINSI YA KUONANA NAE,MUOMBE ANKAL MICHUZI AKUFANYIE MPANGO
    KWA KUWA NIA YAKO NI NZURI KUTAKA KUTUOKOA SISI WATZ,INSHA'ALLAH MWENYEZI MUNGU ATAKUFANYIA UWEPESI NA AKUKINGE NA VITIMBI VYA HAO WENYE ROHO ZA KWA NINI,
    NI KWELI UONAPO MKURUGEZI AU KIONGOZI YEYOTE ANAIJIWA NA MTU MWENYE MAARIFA ZAIDI YA KAZI YAKE,HUWA WANAONA WIVU SANA,LABDA UNGEKUWA WEWE NI NDUGU YAKE ASINGEKUTUMA UENDE KOKOTE,HAPO HAPO ANGEANZA MIKAKATI YA WEWE KUTANGAZA UJUZI WAKO..POLE SANA,MOLA AKUZIDISHIE
    USIKATE TAMAA TAFADHALI!
    AHLAM..LONDON

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 28, 2012

    Ahsante Dr.Sayid A.Sayid

    Pia pole kwa kukatishwa ktk jitihada zako kwa manufaa yetu sote.

    Ndugu yetu ni yako ni njema kwetu na kuna uwezekano mkubwa hao walioziba jitihada zako mwaka 2007 watakuwa wamesha staafu kazi au wamehamishiwa Idara zingine hawapo.

    Kama Wadau walivyosema hapo juu, maradhi makubwa tuliyo nayo wengi wa Watanzania ni:
    -Ubinafsi
    -Dharau
    -Roho mbaya
    -Chuki
    -Tamaa na rushwa
    -Upendeleo
    -Fitina
    -Wivu

    Tafadhali rudi tena ili kwa pamoja tulipeleke suala mbele hata kama itawezekana tutatafuta kila njia.

    Ni wazi kuwa Viongozi wana gawanyika sana hapa nchini, mfano safu ya juu akiwemo mwenyewe Raisi JK ni mpenda maendeleo na hana sifa mbaya hizo hapo juu.

    Ni wazi suala likifika kwake litapata mwelekeo.

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 28, 2012

    We Pimbi nin? Mfumo mfumo mbona huusemi ndio maana ukawa hujapata kuonana na mtu kutokana umeshika Mfumo wa Power point,sasa asojua kutumia power point ni nani?

    Kama maisha yamekubana kajiripue ulipotoka Tanzania haina haja ya mifumo tunaishi kwa nguvu za Mola,huko kwenye mifumo kuna hospitali za vizee kibao wamejaa dementia na diabetic kwa mifumo kama hiyo.

    Watu wengine bwana,au ndio nyie mlosoma vicollege vya wahindi vinafungwa kila siku UK?

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 28, 2012

    Namshauri mdau atumie mtaji wake wa hiyo technology yake kufanya kazi kama majaribio nje ya nchi. Baada ya mafanikio njoo umuone mkuu wa Kaya (JK). Kwa sababu itakuwa ni kitu chenye data za mafanikio somewhere else. Lakini kurudi na theory/idea then uiuze kwa hawa wakuu wetu itakuwa unatwanga maji kwenye kinu. Utapoteza muda mwingi sana. Lakini ukiwa na results then itakuwa ni kazi rahisi kwa mkuu wa kaya (JK) kutoa amri tuu kitu hiki kifanyike pale. Vinginevyo na yeye atakwambia kamuone fulani.

    ReplyDelete
  13. AnonymousJune 28, 2012

    URGENT:
    Kaka michuzi naomba sana unisaidie kupata contact details za huyu jamaa, nahitaji kufanya mahojiano naye muhimu kwa manufaa ya umma kuhusiana na fani yake na mkasa uliompata.
    Nitashukuru akiniandikia kupitia:
    stevejoe25@hotmail.co.uk
    Nitashukuru kwa hilo.

    ReplyDelete
  14. AnonymousJune 28, 2012

    bwana DOC nakusihi tafadhali nakutuma nenda kamuone Balozi wa Diaspora bibie BERTHA usikate tamaa yupo wizara ya mambo ya njee atakupa kazi lazima wakikuletea longo longo yeye mwenyewe ata kupeleka kwa Boss wetu KIJANA MTANASHATI JK

    ReplyDelete
  15. AnonymousJune 28, 2012

    DOCTOR USIRUDI TANZANIA MUDA HUU. UZA PROGRAMU YAKO NCHI ILIYO ENDELA, TENGENEZA MAISHA SAFI HUKO ULIKO HALAFU BAADA YA MIAKA MITANO -- MAMA HAKUKOSEA ALIVYOSEMA 50 -- CHUKUA LIKIZO MIEZI MITATU UJARIBISHE. UKISHINDWA UNARUDI ULIKOTOKA.
    KAMA WENGI WALIVYOCHANGIA HAPO JUU, UNGEKUWA NA CONNECTION, WAKUBWA WAKAJIPATIA TEN PASENTI UNGEPOKELEWA. UTASHANGAA WABABAISHAJI WANAPEWA NAFASI ZA KITAALAMU, WATAALAMU WANAFUNIKWA.
    MIMI NAKUSHAURI WEKA MASLAHI YAKO NA FAMILIA YAKO KABLA YA MTU MWINGINE YEYOTE. UZALENDO TANZANIA ULISHAZIKWA.
    HONGERA SANA NA ALL THE BEST.

    ReplyDelete
  16. Ndugu Dkt. Sayid, Salaam sana. Nimefurahia mno nia yako kurudi nyumbani. Nakupongeza kwa dhati.
    Jambo la kwanza, usiruhusu mtu yeyote akukatishe tamaa kwani nia yako ni nzuri kwako na kwa Taifa la Tanzania. Kukata tamaa ni jambo baya kabisa. Usimruhusu yeyote akukatishe tamaa, wala mimi.
    Jambo la Pili, wapo Watanzania wengi wenye nia njema hapa nchini. Sio Mhesh. Rais peke yake. Watumie watu aliowaweka sehemu mbali mbali walipo na utafanikisha azima yako.
    Tatu, usiweke mbele kupenda kufanikiwa kifedha kwani"Mvumilivu hula mbivu". Umevumilia mengi haswa ukikumbuka kwamba umepitia hatua kadhaa hadi kuifikia "Udaktari wa Falsafa". Mbona zipo njia tele na ukiwatumia Watanzania wengi waaminifu waliopo nchini Tanzania. Tumia vyuo vikuu kwa kuomba nafasi kuwafundisha Vijana. Anzia Nelson Mandela Institute of Science and Technology, kipo Arusha na Vice Chancellor wake ni mtu mchapa kazi mahiri na hana hiana.
    Pia MUHAS, yaani Muhimbili, nako yupo Vice Chancellor makini na mwenye weledi na kiu ya kuona vijana mnashiriki kuijenga Tanzania yetu kwa maarifa yenu.
    Ruka hapo University of Dodoma. Chuo kipya chenye uhitaji wa weledi wa utaalamu kama wako. Vice Chancellor wake ni mwenye ushirikiano mkubwa wa kukuona na kukusikiliza kwa utulivu na maarifa yako yakafika panapohitajika.Hakuna kusota kwenye benchi kama ilivyokuwa pale Wizarani. Mbona wadogo zako wanakuhitaji mno kwa ujuzi na kuwafundisha maarifa uliyo nayo? Kipo sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Huko nako wapo viongozi makini na waliobobea kutumia fursa zilizopo na zijazo, kwa nia ya kuwaendeleza, kuwakuza na kuwawezesha kutumika kadri ya upeo wako. Yaani, mbingu ndio upeo wa utendaji wako katika kutoa elimu. Vyuo vyote nilivyovitaja juu, vinazo websites ambazo ukiandika barua zenye kusudio lako, sawia unajibiwa kuwasilisha vithibitisho vya elimu yako na barua za kuomba kupewa nafasi kujieleza na kuthibitisha utakayosema kwa njia ya Certificates, Diplomas and Degrees. Muhimu wanazuoni kujidhihirisha na vithibitisho.
    Wote hawa wamewekwa na Mkuu wa Nchi kwa niaba yetu sote ili watoe wasomi weledi na wazalendo katika nchi yetu.
    Maoni mengi umepata. Karibu nyumbani tushirikiane kujiendeleza kwa pamoja na tuijenge nchi yetu, Tanzania. MWIKO KURUDI NYUMA WALA KUSITA SITA KUYAFANYIA KWINGINE ILA HAPA KWETU TANZANIA.NGOMA HUCHEZWA KWAKO KWANZA.

    ReplyDelete
  17. AnonymousJune 28, 2012

    Natoa pongezi kwako Dr Sayid kwa jitihada zako za kutaka kuiendeleza nchi yetu, kama walivyosema walionitangulia hapa, mimi sina la kuongeza ila kukutakia kila la kheri kule ni nyumbani lazima tuchangie elimu tuliyo pata huku.

    Kwako Stevejoe25, Dr Sayid anapatikana
    barua pepe
    s.sayid@surrey.ac.uk
    Telephone
    +44 1483 68
    Room
    Postal Address
    Faculty of Engineering & Physical Sciences
    University of Surrey
    Guildford GU2 7XH
    United Kingdom

    Kila la kheri.

    ReplyDelete
  18. AnonymousJune 28, 2012

    Pole sana Dr.Sayid Ally.
    Inshallah siku moja ndoto zako zitatimia na watanzania tutakuwa ni wenye kunufaika kwalo.
    Waweza kutusaidia kupata email yako Dr? kuna jambo nahitaji msaada wa kitaaluma kutoka kwako.

    gadogadian@yahoo.com

    ReplyDelete
  19. AnonymousJune 28, 2012

    Jibu unalo tayari. Umesema walipokuja wazungu kila mtu akapiga salute. Hivyo tafuta mzungu mmoja amechoka choka mvalishe suti nzuri halafu mtie kwenye program.

    ReplyDelete
  20. AnonymousJune 28, 2012

    Ukirudi tena usiishie Wizara ya Afya, waone pia TCRA na Wizara ya Sayansi Teknolojia na Mawasiliano uwaonyeshe hizo slides zako na mfumo wenyewe unavyofanyakazi. Naamini wao wataishauri wizara husika.

    ReplyDelete
  21. AnonymousJune 28, 2012

    Huyo jamaa anatakiwa awe na mahali pa kuanzia hasa kutokana na nchi yetu ilivyo. Ingekuwa vema akaanza kufanya kazi chuo kikuu cha Muhimbili kama daraja la kufikia malengo yake. Lakini pia nashauri apate recomendation toka kwa supervisors wake ili kuipa nguvu proposal yake. Ijapokuwa hatapata kupokelewa kwa haraka ila ana future nzuri sana! Anatakiwa kuwa mvumilivu sana na kuonana na watu wanao matter. Lakini pia anatakiwa anwe na kampuni yake ya IT kwani serikalini lazima kwa tender na siyo kama mashrika binafsi. Kampuni ndio inaweza kuingia mkataba na serikali. Lakini pia anaweza kuanza na hospitali binafsi kama AAR nk. Kazi yake ya hapo inaweza kumtangaza. Lazima kwanza hiyo software ijaribiwe na kukubaliwa. Siyo rahisi kuamini vivi hivyo maana tuko kama Tomaso wote. Bwana songa mbele maana njia iko wazi.

    ReplyDelete
  22. AnonymousJune 28, 2012

    Tanzania kwa kweli ni kuzuri kwa kutembea wiki mbili tu. Nawatembelea na kuwaamkia wazazi, nasalimiana na ndugu na marafiki halafu najirudia Canada. Bongo, maendeleo yanakwenda pole pole sana. Maneno mengi kuliko vitendo. Mpaka leo, maji na umeme hatuna na kadhalika.

    Mimi nimejisomesha na nimejilipia viza yangu mpaka nikawa raia wa hapa. Sina nia yoyote ya kurudi nyumbani.

    ReplyDelete
  23. AnonymousJune 28, 2012

    Wengi wametoa mawazo ya maana (Usijali na wote tumsamehe mtoa comment mmoja aliyeanza kwa kutoa lugha si nzuri bila kutoa ushauri, watu wa aina hiyo wapo katika kila family, jumuia hasa kwenye mtandao). TUNAKUTAKIA MEMA NA UTAFANIKIWA KWA MANUFAA YAKO NA YA WATANZANIA KWA JUMLA

    ReplyDelete
  24. AnonymousJune 28, 2012

    Mdau kwanza Hongera kwa jitihada zako za kusoma kwa bidii na kwa shida kama kila mtu aliyeishi Ughaibuni na akajisomehs mwenyewe anavyojua. Pia pole na kurudi TZ na kisha kurudi tena Ughaibuni mikono mitupu.

    Kwanza naomba uweke anuani ya barua pepe yako hadharani ili wanaoona wanahitaji kukutafuta wakupate kirahisi, kwani hata mimi nahitaji kuwasiliana nawe lkn siwezi kuweka email yangu hadharani kwa kuhofia 'spams', na pia si mimi mwenye shida.

    Pili, HAKIKISHA umesajili project yako (yaani Copyright) hiyo ni muhimu sana, pale BRELA wanasajiri kwa kiasi kidogo tu. Ingawa masuala ya 'Copyright theft' bado hayajaelimishwa sana bongo, zaidi naona kwenye Music Industry tu, lakini niamini mimi kuwa yanakuaja tena kwa kasi. Hivyo sajili ili usije kulia siku moja ukakuta technology hiyo inafanywa na mtu bongo tena ameibadili vibaya mno na mkaishia mahakamani miaka ijayo.

    Tatu, usikate tamaa: Lazima uwe mpiganaji - bongo watu ni wazito kuelewa kupita kiasi, lakini si wote kwani najua wengui walioamua kurudi na Ideas walihangaika vipi na hatimaye sasa wanapeta. Hivyo usitishwe na mtu yeyote yule.

    Nne: 'avoid copycats'. Ingawa point hii ningeiweka hapo juu kwenye Copyright theft, lakini nimeiweka hapa pekee kwa makusudi: Unaweza ukapata 'tender' au ukaanza tu ku-implement hiyo technology yako, lakini watu wakai'chakachua' vibaya mno kisha wakabadili na kutaka kukupiku si kiushindani, bali kukuharibia kazi kwa namna nyingi mno (siwezi kuandika mashairi hapa lakini ningekueleza vipi wajanja wa bongo wanavyoiga mambo na kuharibu).

    Tano: Mtukufu Rais ana kazi nyingi mno jamani kwani kila mtu mwenye idea au technology akitaka kumuona kwa kweli itakuwa ngumu. Unaweza kumuandikia, lakini amini usiamini hatopata muda mwingi wa kuangalia kiundani zaidi (ingawa naweza kuwa 'wrong' hapa), lakini muone Bertha - nadhani kama sijakosea yeye yupo Wizara ya Mambo ya nje na anashughulikia mambo haya ya wana-Diaspora. Hivyo atajua na kukuelekeza ni nini ufanye ili uweze kumuona appropriate person/department.

    Ni hayo tu machache ninayotaka kukueleza.

    PS. Naomba mdau aliyeandika hapo juu kuwa amesoma Computer Eng na Security aandike barua yake pepe nimpatie mtu atayeweza kumsaidia(maybe).

    ReplyDelete
  25. AnonymousJune 28, 2012

    Wewe unaetukana watu na kuwaita Pimbi; Pole sana, nakuonea huruma wewe pamoja na ...

    ReplyDelete
  26. AnonymousJune 28, 2012

    Unategemea nini nchi ambayo kila kitu siasa tu. Hakuna professionalism. We are still in dark ages.

    ReplyDelete
  27. AnonymousJune 28, 2012

    Hongera sana Daktari!

    OMBI LANGU KWAKO NI MOJA TU!

    --> KAMWE usithubutu KUJIINGIZA kwenye SCAM/WIZI kama sasa wafanyavyo baadhi ya watanzania wenzetu wenye PhD kama hiyo yako, iliyopelekea JINA la TANZANIA kuharibika vibaya kama ilivyo NIGERIA.

    Nakutakia kila la kheri

    ReplyDelete
  28. AnonymousJune 28, 2012

    mdau kanivutia, kiswahili chake ni kile kile cha st government school. kwa kweli nimefurahi, ingekuwa wengine hapo kiinglish kingi na kuchanganya lugha. all in all, tafuta "connections" kwanza kabla hujamuona JK, utafika tu!

    ReplyDelete
  29. AnonymousJune 28, 2012

    Uncle , naomba contact za jamaa , nataka kujadiliana nae kidogo kabla hajatua bongo

    amnassir@gmail.com

    ReplyDelete
  30. AnonymousJune 28, 2012

    Pole sana kwa yote hayo yaliyokukuta,Ndiyo maana Tanzania haiendelei inazidi kurudi nyuma,Nchi imejaa mafisadi na rushwa kupita kiasi,ni aibu tupu,nani anayetaka kurudi Tanzania nchi iliyojaa matatizo tu kila kukicha?

    ReplyDelete
  31. AnonymousJune 28, 2012

    sasa mdau unasifia kiswahili chake hajachanganya lugha wakati wewe unachnagnya lugha

    ReplyDelete
  32. Dr Hashim MohamedJune 28, 2012

    Dear Dr. Seyyid Ally Sayyid
    Pole sana. I understand how you feel after what you went through. My name is Dr. Shariff (Seyyid, if you want) Mohamed Abdallah Hashim, medical doctor, retired but no tired. I am the Chairman of the Tanzania Private Health Facilities in Tanzania (APHFTA). This association is an umbrella organisation for the whole Private Health Sector in Tanzania and an important stakeholder in our country. We have nearly 600 members across the country, and growing, commanding a wide range of membership, from small dispensaries to large Tertiary private hospitals as well as 3 Private Medical schools in Tanzania. We have a wide range of programmes to uplift and upgrade business management skills for our members apart from continuous professional development. One of these is to computerize member facilities. Currently we are distributing tablets and desk computers to about 100 facilities across the country and training our members the use of data collection using special software that we have developed. These data are automatically transferred to our saver in Dar es Salaam. You are a kind of guy who can work and find job satisfaction by working with us. You will be most welcome to link with us and we shall provide you with a platform to satisfy your ambition and vision. Please contact me directly or our CEO, Dr Sam Ogillo. We shall be delighted to welcome you to our fold and we can get private health sector to adopt your system. The Public sector in TZ is slow to react to the changing world of IT. Join the private sector. We were planning to import these ideas from our neighbour, Kenya, who are far ahead in computerizing their health systems, but with a Tanzanian offering these ideas to us, we shall be delighted, and promise you full cooperation and support. My email addresses are:
    drsma.hashim@yahoo.co.uk and drsma.hashim@gmail.com.
    Dr. Sam Ogillo is ogillo@aphfta.org OR ogillo@yahoo.com.
    Please get in touch with us now.
    Dr. Hashim. 28 June, 2012.
    Never give up. There is always a way.

    ReplyDelete
  33. AnonymousJune 29, 2012

    Hongera sana Dr.Sayid Ally Sayid na pole kwa yaliyokukuta!

    Isipokuwa uwe makini sana na wimbi la wizi wa haki miliki za kazi.

    Iliripotiwa hasa hasa huko Muhimbili na Taasisi za Kisayansi nchini kumezuka mtindo Ma Dakitari wanaibiana Tafiti na kazi zao

    Hakikisha hiyo kitu kabla ya kuifikisha popote unaisajili kwanza!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...