Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam,Sheikh Issa Ponda,  leo amepanda kizimbani na watu wengine 50 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashawishi baadhi ya Waislamu kuvamia  Kiwanja katika eneo la Chang'ombe jijini Dar es Salaam, kuwashawishi Waislamu kutojitokeza katika zoezi la Uandikishaji katika Sensa ya Watu na Makazi. 
Habari kamili inaandaliwa na itakujia hivi punde
Karandiga lililowabeba Sheikh Issa Ponda na wenzake
Wanahabari wakiwa kazini
Wanahabari wakirekodi kuwasili kwa Sheik Issa Ponda Mahakamani Kisutu leo
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam,Sheikh Issa Ponda,  na watu wengine 50 wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka mbalimbali

Mmoja wa washtakiwa akitelemshwa kutoka kwenye karandinga



Katibu wa baraza la Waislam Tanzania Shekhe Issa  Ponda amepandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam  na kusomewa mashitaka matano.


Alifikishwa mahakamani hapo na kupoandishwa kizimbani na watu wengine 49 akiwemo bibi wa miaka 100 kwa msafara wa magari ya polisi na ving’ora likiwemo gari la maji ya machozi kwa kasi ya ajabu na kushushwa haraka. Hata hivyo baada ya kukana mashitaka yao walirudishwa rumande baada ya kukosa dhamana.

Ponda, aliyewasili peke yake,  alipelekwa moja kwa moja katika chumba cha mahakama na kuunganishwa na washitakiwa wenzake. Wote walisomewa mashitaka hayo mbele ya hakimu Stewart Sanga na wakili wa serikali Jumanne Kweka.

Wote  kwa pamoja walidaiwa kula njama, na katika maelezo ya kosa walidaiwa Oktoba 12, mwaka huu katika eneo la Chang’ombe Markasi katika Wilaya ya Temeke jjijni Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa.

Shitaka jingine wanadaiwa wote kwa pamoja kuingia kwa nguvu kutaka kufanya makosa, huko huko Chang’ombe kwa jinai na bila sababu za msingi walivamia Ardhi katika kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali

Shitaka la tatu walidaiwa kujimilikisha kwa nguvu, maelezo ya kosa walidaiwa wote kwa pamoja walivamia kiwanja hicho pasipo kuwa na uhalali na katika hali ya uvunjifu wa amani, walijimilikisha mali hiyo ambayo ni mali halali ya kampuni ya Agritanza

Aidha katika shitaka la nne ambalo ni la wizi kati ya Oktoba 12 na 16 mwaka huu, washitakiwa waliiba vifaa vya ujenzi walivyovikuta katika kiwanja hicho vyenye thamani ya shilingi 59,650,000 ambavyo ni kokoto, nondo na  saruji mali ya kampuni ya Agritanza.

Shekhe Ponda peke yake ameshtakiwa kuchochea kwa nia ya kuhamasisha utendaji kosa katika maeneo tofauti kati ya Oktoba 12 na 16 mwaka huu, kama katibu wa baraza la Waislam Tanzania, huko Temeke eneo la Chang’ombe, jijini Dar es salaam.

Washtakiwa wote walikana mashtaka hata hivyo walirudi rumande kwa sababu hakimu aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo hakuwepo na hivyo kusomwa mbele ya hakimu Sanga ambaye alisema hana mamlaka.

Mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana ya Shekhe Ponda kwa kile alichotaja kuwa ni kwa usalama wa Ponda na pia kwa maslahi ya Jamhuri.  Kesi hiyo itatajwa Novemba mosi mwaka huu na kwamba upelelezi haujaamilika.

Pamoja na jitihada za wakili wao Juma Nasoro kuwaombea dhamana wateja wake lakini jitahada hizo ziligonga mwamba.

Msafara wa zaidi ya magari kumi uliondoka na washitakiwa hao huku likiwemo gari lile la maji ya machozi maaskari wa barabarani, askari magereza na fidifosi huku Ponda akiwekwa katika gari la vioo vya giza kama alivyoletwa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. Inshaallah kwa uwezo wake mola mtatoka soon jela sio sehemu nzuri.

    ReplyDelete
  2. Hii ni njaa tu inatusumbua Waislamu; sasa tukichoma makanisa tutapata nini kama siyo kuwapa jamaa sababu za kutuweka ndani? Tutafuteni maendeleo; mimi ndiyo maana nilihamia Rwanda, njooni huku, nafasi zipo lakini shule lazima. Hata Burundi nafasi kibao, Watanzania huku tunapendwa, siyo kama tukienda Kenya na Uganda. Poleni sana.

    Moody.

    ReplyDelete
  3. Naomba kutoa ushauri kwa waandishi kuwa makini kwani wanapo andika suala lolote lile linalohusu kundi fulani la waumini wa kiislamu wao huandika kwa kutumia "Waislamu" kwa ujumla hii nikuleta sura fulani ya waumini wa dini hii, aidha kwa kukusudia kutimiza ajenda fulani au ukosefu wa mtazamo wa kina juu ya maandishi yao. Kutunza amani ya Taifa ni jukumu letu wote tuwe na hadhari ya maandishi yetu. Hivi kwani hatuandiki "mkristo" akojolea Msahafu na tuna andika mtoto bila kuainisha dini yake? Tujaribu kuwa waadilifu. Nakupenda nchi yangu Tanzania

    ReplyDelete
  4. Mtu yoyote ambaye hafuati mafundisho ya Yesu siyo mkristo. Sasa huyo mtoto wamuandike mkristo ya vigezo vipi? Na wasiwasi na elimu yako wewe mdau.

    ReplyDelete
  5. Hao ni waislaam wenye msimamo wa kipuuzi. Kama kitu kidogo kilichofanywa na mtoto asiyekuwa na malezi mazuri kimewafanya watu wenye akili timamu wachome makanisa nane? Huu ni kutokuwa na elimu ya kutosha....sasa ngoje niwaulize swali moja...Huyo mtoto mpuuzi aliyekojolea msahafu anahusika vipi na hayo makanisa nane tofauti tofauti ya kikristo? TUKUE JAMANI!

    ReplyDelete
  6. Watetezi wa haki za binadamu mko wapi? Watu bado wanapandishwa kwenye malori? Huu sio ubinadamu. Yaani hata basi la maana lenye viti limeshindwa kupatikana?

    ReplyDelete
  7. Kuna mdau ametoa pointi nzuri kuhusu vichwa vya habari. Vichwa vya habari huenda vingekuwa sahihi zaidi kama vingekuwa vinasema kitu kama 'kundi la waislamu lavunja makanisa' maana kuna waislamu wengi tu ambao wanaheshimu utawala wa sheria na ambao wangeweza kufuata sheria kupata haki wanayoamini wanaistahili.
    Kwa upande wa mtoto lakini waandishi wanaandika mtoto akojolea msahafu kwa sababu aliyekojolea msahafu ni mtoto. Mtoto anaeleweka ni binadamu ambaye bado hajafikia hatua ya kufanya maamuzi ya maisha yake. Ndiyo sababu hata kura hawapigi, hawatakiwi kufanyishwa kazi kwa maana ya 'child labor', hawatakiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara na wazazi wao wanatakiwa kuwapatia mahitaji ya msingi. Kumtambulisha mtoto kwa imani fulani ni kujifurahisha tu ndio sababu watu wengi huamua kubadili dini wanapokuwa watu wazima.
    Tatizo lakini sio vichwa vya habari. Tatizo ni tukio. Kundi la Waislamu limeghadhabishwa(and rightly so) na kitendo cha mtoto kukosa heshima kwa kitabu kinachoongoza imani yao. Kwa hasira wanaenda kuvunja makanisa randomly. Sasa unapovunja kanisa la Wasabato au Wakatoliki, tena ambalo huyu mtoto hata haendi kusali maana yake ni nini?
    Kuna watu kibao wanasubiria kisingizio kidogo tu waanzishe vagi. Vagi limebumburuka Waziri Mkuu katimkia zake Uingereeezaaa!

    ReplyDelete
  8. Nakubaliana na wadau hapo juu hasa wewe uliyesema watafute kazi kwa jirani zetu LAKINI ELIMU! Nawe ulieleza kuwa kuhusu makundi fulani ambayo yapo kuanzisha vurugu ili wavamie na kupora mali za watu na makanisa, jamani TUNAUTIA AIBU UISLAMU, TUACHANE NA HAYO, KWA NINI TUNAHUKUMU? Naamini mtoto huyu alikwisha kutubu na kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ole wetu tunayoyaendelezaa na kuyakuza!!!. KAZI, KUJISHUGHULISHA, n.k. ndiko kunatuletea haya yote. Tusisingizie ajira, hatutaki kujishughulisha kila siku. Mimi nawapongeza sana wakina mama ambao wameamua kufanya biashara za matunda mimi kila niwaonapo hupenda kuwasupport kwa kununua bidhaa zao. Tuache UVIVU NA TUCHAPE KAZI. Hizi ninyi wenzetu mngekuwa na shughuli ya kufanya sidhani kama mngeweza kutokea kwenye UPUUZI ambao unasabisha WAISLAMU wooote tuonekane HOVYO! Njia rahisi ya kujikomboa kwenye hii hali ngumu ya maisha ni kuchapakazi na kuukataa UMASKINI NA KIJIELIMISHA KIKWELIKWELI NA FAIDA ZAKE TUTAZIONA NA WALIJIBIDISHA KWA BIDII.

    ReplyDelete
  9. Wakazi wanaoishi mbagala eneo la tukio wanafahamu huyo kijana mwenye miaka 14 mwanafunzi wa sekondari ni mkristo, ndio maana mdau kaandika mbona haiandikwi mristo kakojolea msahafu. Kwa KIGEZO hicho, majirani zake wanamfahamu. Sasa ukiuliza kwa kigezo gani hatukuelewi.

    ReplyDelete
  10. Wadau hilo ni genge tu la wahuni na vibaka,si mmeona vitu vyao visivyoenda shule............. Subiri waipatepate fresh ya Mkono mrefu wa sheria.

    ReplyDelete
  11. ndugu Moody weka email yako hapa ili tuweze kuwasiliana nawe kupata info zaidi za namna ya kuja huko uliko.

    Thanks

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...