MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la dunia (Miss World), Brigitte Alfred, amefanya kweli baada ya kufanikiwa kutwaa nafasi ya tatu katika shindano dogo la Beauty with a Purpose.
 
Brigitte aliye Redd’s Miss Tanzania 2012/2013, anatarajiwa kupanda jukwaani leo huko Bali, Indonesia, kuwania taji la Miss World.
 
Taji la Beauty with a Purpose limetwaliwa na Ishani Shrestha wa Nepal na kilichomfanya Brigitte ashike nafasi hiyo ni kutokana na video aliyoiwasilisha kuhusu kazi alizofanya kwa jamii hapa nchini.
 
Video hiyo hapo chini aliyoiwasilisha Brigitte ilionyesha kazi ya jamii aliyoifanya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi - albino.
 
Nafasi ya pili ilichukuliwa Erin Holland wa Australia, huku lile la ‘Top Model’ likitwaliwa na Megan Young wa Ufilipino, Jacqueline Steenbeek wa Uholanzi akatwaa la michezo, Sancler Frantz wa Brazil akachukua la ‘Beach Fashion’, Vania Larissa wa Indonesia alitwaa la Miss World Talent na Navneet Dhillon wa India akatwaa la Multimedia.
 
Washindi watano katika mashindano hayo madogo wana uhakika wa kuingia hatua inayofuata, huku Brigitte kwa nafasi hiyo ikiwa imemsaidia kwa kiwango kikubwa kujiamini kwa kusonga mbele.
 
Brigitte anashiriki fainali leo, huku akiwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anafuata nyayo za Nancy Sumari aliyefanikiwa kutwaa taji la Afrika katika mashindano ya Miss World ya mwaka 2005.
 
Akizungumza kutoka Indonesia, Brigitte alisema, wengi walifurahi kazi yake aliyopeleka ambayo ilionyesha pia kwa kiasi kikubwa jinsi watu wenye ulemavu wa ngozi wanavyohitaji msaada, hasa kutokana na kuwindwa na baadhi ya watu.
 
“Waliipenda kazi yangu, lakini kwa shindano la kesho (leo) nina uhakika mkubwa wa kufanya vizuri, kwani vigezo vyote ninavyo na nimejiandaa kwa muda mrefu mno.
 
“Niseme wazi nimejiandaa kwa muda mrefu mno na nashukuru wote walionisaidia kwa njia moja au nyingine na hii inanipa moyo wa kufanya vizuri zaidi,” alisema.
 
Wakati akimuaga Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alimtaka ahakikishe anaipeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kufanya vyema katika mashindano hayo.
 
“Fahamu fika kwamba unakwenda Indonesia kama Miss Tanzania na si Brigitte, hivyo unatuwakilisha Watanzania wote, sisi tuko nyuma yako unachotakiwa ni kujiamini tu na utafanikiwa.”
 
Mrembo huyo alifanikiwa kulitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania mwishoni mwa mwaka jana, akitokea kitongoji cha Sinza na Kanda ya Kinondoni.
 
Taji la Miss World linashikiliwa na mrembo Wenxia Yu kutoka China, ambaye tayari alikuwa Indonesia kwa ajili ya kulivua taji hilo.
 
Redd’s Miss Tanzania kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Lundenga alisema kuwa Brigitte ambaye pia ni Miss Sinza aliweza pia kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini na sura nzima ya Tanzania katika mashindano hayo makubwa ya urembo duniani.

 “Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kufanya vyema katika mashindano ya dunia  baada ya Nancy Sumari mwaka 2005 alipomaliza katika fainali ya warembo tano bora kati ya warembo 120 duniani. Nancy alishinda taji la mrembo bora wa Afrika, hivyo Brigitte ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri  leo katika fainali mashindano hayo (Miss World) yanayofanyika mjini Bali, Indonesia, naomba tumuombee aibuke kidedea,” alisema Lundenga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...