Na Abushehe Nondo, Maelezo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi, Edwin Ngonyani amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi na kumlipa fidia ya shilingi bilioni moja kutokana na kuandika habari ya kumchafua.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake Waziri Ngonyani amesema kuwa Gazeti hilo la tarehe 4 Agosti 2016 liliandika habari yenye kichwa cha Habari “Waziri amchafua JPM” ikimuhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya Kampuni ya Madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

“Nimewaandikia notisi ya siku saba ikiwataka waombe radhi na kunilipa fidia, na wasipofanya hivyo hatua stahiki kuwapeleka mahakamani akiwemo Mwandishi Josephat Isango, Mwanahalishi Publisher na Mchapaji wa gazeti hilo”. Alisema Mhandisi Ngonyani.

Mhandisi Ngonyani amesema kuwa habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia nyaraka za kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa tarehe 24 Julai  na kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO wakati ukweli ni kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili na siyo Kaimu kama barua hiyo inavyosomeka.

Ameongeza kuwa habari hiyo imewachafua watu wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake wa jimbo la Namtumbo ambao walijitoa katika kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika zimemchafua Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhusisha na fedha kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini itakuwa salama.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alishasema kama kuna mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake ikulu ajitokeze na hakuna aliyefanya hivyo, Iweje leo mtu tu anaibuka na kuandika habari za kugushi? ”. Aliongeza.

Aidha Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kuwa waangalifu pindi wanapoandika habari za kutunga kwa kutotumia majina halisi kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni za uandishi wa hadithi (Habari za kutunga).

“Waandishi wa habari mnatakiwa kufuata maadili ya kazi yenu kwa kuandika habari zenye ukweli ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko na  migogoro isiyo ya lazima” Alisema Naibu waziri huyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...