THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

HAL yafanya kazi miaka 8 bila kibali cha TBS

KAMPUNI inayojulikana kama Hanspaul Automechs Limited (HAL) iliyopo Arusha imekuwa ikifanya kazi nchini kwa takriban miaka nane sasa bila kuwa na idhini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

HAL ilianzishwa mwaka 2007 ikijishughulisha na utengenezaji na uuzaji ndani na nje ya nchi mabodi ya magari maalumu kwa safari za kitalii maarufu kama ‘Safari’.

Hayo yamefahamika hivi karibuni baada ya TBS kuthibitisha kuwa haijawahi kuipa HAL cheti cha ubora kwa ajili ya mabodi hayo, hivyo kuliweka njiapanda shirika hilo katika vita vya kusaka haki ya kutengeneza mabodi hayo yanayofahamika pia kwa jina la ‘War Bus’.

Kesi ya kutafuta haki hiyo ipo mahakamani kwa muda mrefu sasa kati ya HAL na kampuni nyingine ya utengenezaji mabodi ya aina hiyo iliyopo Mjini Moshi, RSA Limited, ambao wanadai wao ndio wabunifu wa awali wa mabodi hayo.

Wiki iliyopita, kilifanyika kikao kwenye Makao Makuu ya TBS jijini Dar es Salaam chini ya Mwanasheria wa Shirika hilo, Humphrey Shonga, kati ya maofisa wa TBS na wanasheria wa RSA Limited.

Katika kikao hicho cha Agosti 18 mwaka huu, wanasheria wa RSA Limited walihoji sababu za TBS kuruhusu bidhaa zisizokuwa na cheti cha ubora kuingizwa katika soko la Tanzania na pia kuuzwa nje ya nchi zikitokea Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao hicho, ili TBS iweze kuwapa HAL cheti cha kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, waliwaagiza kuwasilisha vielelezo na michoro ya utengenezaji wa mabodi hayo ambavyo haviendani na vya mshindani mwingine yeyote.

“HAL wameshindwa kuwasilisha vielelezo hivyo hadi leo,” alisema mmoja kati ya watu waliohudhuria kikao hicho ambaye hakupenda jina lake liandikwe na kuongeza:

“Hata hivyo, pamoja na kutotambuliwa na TBS, HAL imekuwa ikipata upendeleo wenye shaka wa kutengeneza na kuuza ndani na nje ya nchi bidhaa hizo.”

Barua ya Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA) kwa wanasheria wa RSA Limited ya Julai 25 mwaka huu, inaweka wazi kuwa, Februari 24, 2016, HAL ilipewa leseni ya muda (Temporary Industrial License) namba 00000928 ikitakiwa kuwasilisha taarifa ya maendeleo za kila mwaka huku bidhaa zinazozalishwa zithibitishwe ubora na TBS.

“Hii inathibitisha kuwa kwa miaka nane, HAL imekuwa ikibadili na kutengeneza mabodi ya magari ya kitalii bila kuwa na leseni huku mamlaka husika zikishindwa kuchukua hatua,” alisema mtoa habari wetu.

Kwa mujibu wa kanuni za TBS na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), magari yote yenye dhamana ya kubeba abiria lazima yathibitishwe na TBS kabla ya kuingia barabarani.

“Lakini hadi sasa TBS haijaonyesha nia ya kutekeleza kanuni hiyo kwa walau kuionya HAL kwa kosa la kuingiza bidhaa zake sokoni bila kibali chao, au kuuambia umma kwmba mabodi yao (Safari Tourist Bodies) ni salama na halali kubeba abiria au la,” alisema.

Ukimya wa TBS unazidisha shaka kwa sababu ni wazi kuwa maofisa wao waliopo kwenye mipaka kama Namanga, Sirali au Mutukula na wengine wanaofanya ukaguzi maeneo mbalimbali nchini wamewahi kukutana na bidhaa za HAL.

“Au basi hata barua za RSA Limited za mwaka 2008, 2014, 2015 na 2016 (nakala zake tunazo) kuitaarifu TBS suala hili, zingetosha kuwaamsha wakaguzi wa shirika hili muhimu kwa afya na usalama wa Watanzania na kuchukua hatua,” alisema.

Alipotafutwa jana kwa njia ya simu kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi, Afisa habari wa TBS, Bi Rhoida Andusamile alisema hawakuwa tayari kuizungumzia swala hilo kwani shirika hilo ilikuwa katika maandalizi ya kutoa taarifa rasmi hapo baadaye, bila kutaja ni lini taarifa hiyo itatoka.

Kwa upande mwingine, HAL pia imekuwa ikipata mauzo makubwa kwa kuungwa mkono na Toyota Tanzania Limited (TTL) inayotambua bidhaa hizo wakati ubora wake haujathibitishwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa HAL Group, Satbir Hanspaul, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha kati ya mabodi (war bus) 30 na 35 kwa mwezi lakini hutengeneza mabodi aina ya Winnebago kwa oda maalumu.

Mwaka jana, Hanspaul aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kenya, Uganda na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazoagiza 'War Buses' kutoka Arusha kwa ajili ya kusafirisha watalii kwenye mbuga zao.

Zipo taarifa kuwa mataifa mengine ya ughaibuni huagiza mabodi yaliyotengenezwa maalumu na kampuni hiyo kwa ajili ya kutumiwa na majeshi ya huko.


Kuna Maoni 2 mpaka sasa.

  1. Hawa wasikatishwe tamaa bali wawezeshwe kupata certification za TBS na WAPEWE USIMAMIZI WA KARIBU utakaowawezesha kufanya kazi zao vyema na kuuza bidhaa zao kimataifa.

  2. Anonymous Anasema:

    Naunga mkono wasikatishwe tamaa hasa wakati huu ambapo tunapigania viwanda. Kama wamekuwa wakiuza hata nje ya nchi kwa miaka yote hiyo ni bora wamalizane na TBS na kuendelea na mzigo.