THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

ANDAENI WATAALAMU WA KUTOSHA-WAZIRI MKUU MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iweke mpango maalumu wa kuongeza wataalamu zaidi katika sekta ya afya ndani ya nchi ili kuipunguzia Serikali gharama za kusomesha wataalam hao nje ya nchi.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 2, 2016) wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha Muhimbili katika eneo la Mloganzila.

Amesema Serikali zilizotangulia zimefanya kazi kubwa na nchi imefikia hatua nzuri ya kuongeza wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda kutatua changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa kwenye hospitali za mikoa na wilaya.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha tiba cha kimataifa pia utawapunguzia wananchi adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata matibabu nje ya nchi. Tayari upasuaji mkubwa wa magonjwa ya moyo umeanza kufanyika nchini. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bw. Humphrey Polepole awasake watu wote waliohusika na wizi wa lita 1,000 za mafuta ya kuendeshea mitambo katika karakana ya mkandarasi anayejenga Kampasi hiyo.

“Wafanyakazi waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje katika karakana ya mkandarasi? Hii kampuni inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na Mkuu wa wilaya usimhurumie mwizi,” amesisitiza.Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kukamilika kwa kampasi ya Mloganzila kutasaidia upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini ambao watapunguza gharama za kupeleka wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Ephata Kaaya alisema kukamilika kwa hospitali pamoja na kampasi yote ya chuo kutawezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa wataalamu wa afya nchini.

Amesema hospitali hiyo itatumika kutoa huduma za afya za kitaalam zaidi kwa magonjwa mbalimbali, hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Pia itapunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ujenzi wa mradi huo umegharimu Dola za Kimarekani milioni 61, ambapo Serikali imetoa Dola milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa Dola milioni 43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Mloganzila kutawezesha chuo kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya afya kutoka 4,010 hadi 15,000.

Prof. Kaaya amesema mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ulisainiwa tarehe 12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi Julai, 2015 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM. 
IJUMAA, SEPTEMBA 2, 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akitaza mashine ya CT Scanner wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila jijini Dar es salaam Septemba 2, 2016. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akikagua jiko wakati alipolea eneo ilipojengwa Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila jijini Dar es salaam Septemba 2, 2016. Watatu kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Tekinolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Ephata Kaaya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiondoka baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Kampasi Mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) eneo la Mloganzila jijini Dar es salaam Septemba 2, 2016. Kulia kwake ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Tekinolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Humphrey Polepole .