THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

MAKAMU WA RAIS KUZINDUA JENGO LA MAADILI, MTWARA.

Joseph Ishengoma.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasani tarehe 8/9/2016 anatarajia kuzindua jengo la Maadili kanda ya Kusini Mkoani Mtwara.

Jengo la Maadili limejengwa kwa awamu tatu na kampuni za ujenzi za M/s Price General Investment Ltd, M/s G. Engineering &Construction Co.Ltd na M/s AC Technology Ltd kwa gharama ya shilingi 2,139,214,906.88 chini ya usimamizi wa Wakala wa majengo nchini TBA.

Kati ya gharama hizo, shilingi 116,000,000 ni kwa ajili ya ushauri wa mradi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara leo, Kamishna wa Maadili Jaji (Mstaafu) Salome Kaganda amesema kuwa fedha zote za mradi wa ujenzi  huo zimetolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 “Naishukuru Serikali kwa kugharamia ujenzi huu kwa asilimia 100, kwasababu kutokana na unyeti wa kazi tunazofanya hatupaswi kuwa katika nyumba ya kupanga. Kupanga nyumba kunatusababishia ugumu katika utendaji kazi,” amesema.

Tangu mwaka 2005 Sekretarieti ya Maadili ilipofungua ofisi ya Kanda ya Kusini inayohudumia mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi, ilikuwa ikipanga katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa mkoa Mtwara.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Maadili, kuwepo kwa jengo hilo kutasaidia kuboresha utendaji kazi  wa Sekretarieti na idadi ya watumishi kwa ajili ya kutoa huduma itaongezeka.

Aidha Jaji Kaganda ameiomba Serikali kujenga  ofisi nyingine za maadili katika kanda sita zilizobaki ili kuondokana na adha ya nyumba za kupanga. Sekretarieti ina ofisi nyingine katika kanda ya Ziwa, kanda ya Kaskazini, kanda ya Mashariki, Kanda ya Kati, Nyanda ya juu kusini na Kanda ya Magharibi.

“Serikali ikubali kujenga majumba mengine ili tuondokane na nyumba za kupanga. Tukipata majengo yetu, kazi itafanyike kwa mujibu wa taratibu za maaadili,” amesema.
Kamaishna Kaganda ametoa wito kwa viongozi, wananchi na wadau mbalimbali kutoka mikoa ya Kusini na Tanzania kwa ujumla kufika katika ofisi za maadili ili wahudumiwe na kuisaidia Sekretarieti kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma nchini.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ilianzishwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria ya Maadili namba 13 ya mwaka 1995 kusimamia maadili ya viongozi nchini.