Na Cathbert Kajuna.
First
National Bank Tanzania (FNB) imezindua rasmi mashine za malipo kwa njia
ya kadi (POS Devices) jijini Dar es salaam kama hatua ya kuimarisha
matumizi ya kadi za benki kwa ajili ya malipo ya bidhaa na huduma kwa
njia salama, rahisi, na kwa gharama nafuu na zitatumika kama mbadala wa
fedha taslimu. Mkuu wa bidhaa na huduma za dijitali wa benki hiyo,
Silvest Arumasi alisema benki itatoa mashine za kuweka maeneo mbalimbali
ya biashara kubwa na biashara ndogo au za rejareja.
Vilevile
benki hiyo itatoa mashine ndogo za kubeba kama simu ambazo zitatumika
kwenye sekta ya utalii na mahoteli pamoja na biashara nyingine hasa zile
zinazohama hama kwani mashine hizo zinatumia mtandao wa Intaneti kama
simu. “Biashara yoyote inaweza kutumia mashine za malipo kwa njia kadi
(P0S Device) kupokea malipo ya bidhaa au huduma.
Huduma
hii inatarajiwa kuongeza tija kwenye maeneo ya biashara kwa kupunguza
hatari zitokanazo na utunzaji fedha taslimu na pia itapunguza safari za
wafanyabiashara kwenda katika matawi ya benki kuweka fedha na sasa
wataweza kutumia muda mwingi zaidi kuendesha biashara.
Mashine
za malipo kwa njia ya kadi zinaweza kuwekwa sehemu ya kudumu karibu na
wateja au kubebeka kulingana na mahitaji ya mteja” alisema. Alisema
kuanzishwa kwa huduma hiyo kutaboresha huduma za kidijitali za benki
hiyo kwani sasa wateja wataweza kuangalia na kupakua taarifa za mihamala
na fedha kila siku na za kila mwezi jambo ambalo litawasaidia
wafanyabiashara katika kutunza mahesabu. Uzinduzi wa mashine hizo ni
sehemu ya mkakati wa FNB kuwa kiongozi katika huduma za benki na sehemu
ya mpango wa benki hiyo kuchangia ukuaji wa uchumi kwa kuwawekea
wafanyabiashara mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao.
Arumasi
alisema kuwa sambamba na uzinduzi huo, benki hiyo imepokea tuzo ya
ufanisi wa kadi za fedha na malipo za VISA kwa mwaka 2016 baada ya kuwa
imekidhi viwango vya ubora kimataifa na kuwa benki bora nchini katika
utoaji wa huduma kupitia kadi hizo. Hii ni kutokana na huduma bora kwa
wateja, ufanisi, na mfumo wa kuaminika katika kuendesha shughuli za
kibenki.
Programu
ya tuzo za viwango vya ubora za VISA kimataifa ilianzishwa mwaka 1992
ili kutambua taasisi za kifedha dunia nzima zinazotoa huduma bora kwa
watumiaji wa kadi za VISA kwenye maeneo mbalimbali. Kila mwaka tuzo hizo
utolewa kwa taasisi hizo kutokana na kukidhi viwango vya ubora katika
utendaji, ufanisi na mifumo madhubuti ya kudhibiti udanganyifu.
Meneja Masoko wa First National Bank Tanzania, Bi. Blandina Mwachang’a (Kushoto), na Mkuu wa kitengo cha bidhaa na huduma za kimtandao, Bw. Silvest Arumasi ( kulia) wakionyesha Mashine za malipo kwa njia ya kadi ambazo benki hiyo imezindua ili kuimarisha matumizi kadi za benki kama mbadala wa fedha taslimu Katikati ni Meneja wa Huduma za Kadi, Bi. Emma Kilimba akiwa ameshikilia tuzo ya ufanisi wa mashine hizo za malipo kwa mwaka 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...