Klabu ya
Rotary ya Oyster Bay ya jijini Dar es Salaam imekabidhi rasmi ukuta uliojengwa na
klabu hiyo katika Shule ya Msingi ya Msasani A na Msasani B. Ukuta huo
umejengwa ili kuimarisha usalama kwa wanafunzi wa shule hizo pamoja na kulinda
mali za shule. Kabla ya ujenzi wa ukuta huo, mazingira ya shule hizo yalikuwa
hatarishi kwa wanafunzi kutokana na watu wasiohusika kupita katika eneo la
shule bila udhibiti.
Ujenzi wa
ukuta huo wenye thamani ya takribani Tshs Milioni 35 umewezeshwa na fedha
zilizopatikana kutoka kwenye mojawapo ya shughuli za uchangishaji fedha
zinazofanywa na klabu hiyo ambapo wadau mbalimbali walichangia ili kufanikisha
zoezi hilo.
Ukuta
huo ni muendelezo wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Klabu ya Rotary ya
Oyster Bay katika kuboresha mazingira ya shule hiyo. Jitihada nyingine
zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa maktaba mbili pamoja na kuweka vitabu vya
aina mbalimbali, maji safi na salama ya kunywa, kambi ya siku moja ya huduma za
bure za upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali, mafunzo kwa walimu pamoja
na upandaji wa miti.
Hafla
hiyo fupi ilihudhuriwa na wanachama wa klabu ya Rotary ya Oyster Bay pamoja na
viongozi wa ngazi ya juu wa Muunganiko wa Klabu za Rotary katika nchi za
Tanzania na Uganda. Kiongozi Mkuu wa mkusanyiko wa klabu za Rotary Tanzania na
Uganda, bwana Jayesh Asher alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo na
alipongeza juhudi za klabu ya Oyster Bay katika kusaidia shule hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...