Mkurugenzi Stephen Magoiga
Na Mwandishi Maalumu, Kishapu

Mkuu wa Shule ya Sekondari Shinyanga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Marxon Paul amevuliwa madaraka kutokana na tabia ya ulevi na kushindwa kusimamia taaluma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga alichukua hatua hiyo baada ya kufika shuleni hapo na kukuta mgomo huo uliochangiwa na tabia ya mkuu huyo.

Akithibitisha hatua hiyo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari halmashauri hiyo, Paul Kasanda alisema kuwa mkuu huyo ameshindwa kuwasimamia walimu anaowaongoza.Kasanda alisema kuwa kutokana na kushindwa kuwasimamia walimu hao kumewafanya wajiamulie wenyewe mambo yao na hivyo kutofundisha ipasavyo hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa taaluma shuleni hapo.

“Ni kweli mkurugenzi jana baada ya kutembelea shule hiyo na kupata malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi, amechukua uamuzi wa kumvua madaraka mkuu wa shule,”alisema.Kaimu Mkuu huyo wa Idara ya Elimu Sekondari aliongeza kuwa tabia ya mkuu huyo imekuwa haivumiliki na kuwa maamuzi yaliyochukuliwa na mkurugenzi ambaye ni mwajiri wake ni sahihi.

Alibainisha kuwa shule hiyo ambayo ni ya wavulana ya bweni imekuwa ikiporomoka siku hadi siku kutokana na kuwa na uongozi ambao haufanyi kazi yake ipasavyo.“Tumeona tuchukue hatua stahiki dhidi ya mkuu huyo wa shule ili iwe fundisho kwa wengine, hebu fikiria kiwango cha ufaulu kimekuwa kikishuka kila mwaka tangu 2012 katika mitihani mbalimbali wanayofanya wanafunzi,” alisema Kasanda.

Kwa sasa shule hiyo inaongozwa na Makamu Mkuu, Mwalimu Marco Badalaha hadi pale uteuzi mwingine kuziba nafasi hiyo utakapofanywa na Katibu Tawala wa Mkoa.Hatua ya mkurugenzi mtendaji kuwaondoa watumishi wazembe ni mojawapo jitihada zilizoanzishwa na Rais Dk. John Magufuli ili kuleta ufanisi katika utendaji serikalini.

Ikumbukwe hivi karibuni, alipowateua wakurugenzi wa mamlaka mbalimbali nchini, Rais Magufuli aliwapa meno ya kuwachukulia hatua watumishi wanaokiuka maadili bila kuogopa. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...