Na Asteria Muhozya, DSM

Wizara ya Nishati na Madini, imeandaa Mkutano ambao pamoja na masuala mengine utapokea Taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, ambao utahudhuriwa na Mawaziri wanaosimamia sekta hiyo kutoka Uganda na Tanzania.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Jijini Tanga tarehe 24 hadi 26,Oktoba, 2016, utatanguliwa na mkutano wa Wataalam kutoka Serikali ya Tanzania na Uganda na kisha kufuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa sekta hizo, na tarehe 26 Oktoba, 2016, utafanyika Mkutano wa Mawaziri wa nchi husika.

Mbali na Wataalam kutoka Tanzania na Uganda, mkutano huo pia utashirikisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Wawekezaji katika mradi huo kutoka Kampuni za Total E&P ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza, China National Offshore Oil Company (CNOOC) na kampuni za Mafuta za Taifa za Tanzania na Uganda.

Mradi wa bomba hilo una urefu wa kilomita zipatazo 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Bomba hilo linatarajiwa kupita katika mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Shinyanga Dodoma na Tanga.

Mradi huo ambao uliridhiwa na Baraza la Mawaziri kutekelezwa nchini Tanzania mnamo tarehe 29/09/2016, katika kikao kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, utakua na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa kuongeza kasi ya kukua kiuchumi.

Bandari ya Tanga itapata fursa za kuongeza kiwango cha kufanya biashara na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi na hivyo kuweza kufungua mkuza wa kiuchumi baina ya Mikoa ambayo bomba hili litapita na nchi Jirani za Afrika Mashariki.

Mradi huo unaotajwa kuwa mradi mwingine wa kihistoria, utagharimu kiasi cha Dola za Marekani takribani Bilioni 3.5, ambapo utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafirisha jumla ya mapipa Laki Mbili (200,000) kwa siku. Mradi utakua na Manufaa kwa Taifa ikiwemo kutoa ajira za muda mfupi na mrefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...