Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akisalimiana na Ahmed Olotu(Mzee Chilo) mara baada ya kupokea shilingi laki sita na ishirini kutoka kwa Mtandao wa wasanii(SHIWATA) ikiwa ni msaada wa kusaidia waathirika wa tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera.Wengine pichani ni Mkurugenzi Idara ya uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Gen.Mbazi Msuya na Caasim Taalib(wa tano kushoto) ambaye ni Mwenyekiti wa mtandao wa wasanii.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara ndogondogo solo la kariakoo mara baada ya kupokea msaada wa nguo mchanganyiko,midoli na kanzu wenye thamani ya shilingi milioni 2 ikiwa ni msaada wa kusaidia waathirika wa tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera.

……………………………………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu sh. milioni 25.62 pamoja na nguo zenye thamani ya sh. milioni mbili kutoka kwa wadau mbalimbali.

Makabidhiano ya michango hiyo yamefanyika leo (Ijumaa, Oktoba 14, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akiwashukuru wadau hao Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Nawashukuru kwa kuamua kutumia siku ya leo ya kukumbuku ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa,” amesema.

Waziri Mkuu amesema michango hiyo ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo baina ya Watanzania.

Misaada hiyo imetolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sh. milioni 20, Mtandao wa Wasanii Tanzania sh. 620,000 na nguo mifuko miwili, Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA) sh. milioni tano.

Wengine ni Umoja wa Wafanyabiashara Ndogondogo soko la Kariakoo ambao wametoa marobota mawili ya nguo (suruali, kanzu na nguo za akinamama na moja la wanasesere kwa ajili ya watoto waliopatwa na maafa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni mbili.

Fedha na nguo hizo vimetolewa kwa ajili ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...