Na Veronica Simba
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewakaribisha
wawekezaji kutoka Italia, kuja kuwekeza nchini hususan katika sekta ya
nishati.
Profesa Muhongo alitoa ukaribisho huo kupitia kwa Balozi wa Italia hapa
nchini, Roberto Mengoni, aliyemtembelea Waziri ofisini kwake jijini Dar es
Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo baina yao.
Waziri Muhongo alimweleza Balozi Mengoni kuwa, zipo fursa nyingi za
uwekezaji hapa nchini katika sekta ya nishati ikiwemo uzalishaji wa umeme
kwa kutumia vyanzo mbalimbali ambavyo alivitaja kuwa ni gesi asilia,
makaa ya mawe, jotoardhi, upepo, tungamotaka, mawimbi ya bahari na
maji.
Aidha, alitaja fursa nyingine ya uwekezaji kuwa ni katika Bomba la
kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki, litakalotoka Hoima Uganda
hadi Tanga nchini Tanzania.
Hata hivyo, Profesa Muhongo aliweka bayana kuwa, fursa zote za
uwekezaji zitatolewa kwa njia ya ushindani wa wazi.
Awali, akieleza madhumuni ya kumtembelea Waziri; Balozi Mengoni
alisema Italia ingependa kuwekeza katika sekta za nishati na madini nchini
ili pamoja na mambo mengine, kuendeleza na kuimarisha uhusiano mzuri
uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo pia kuiomba Italia, ufadhili wa
masomo yanayohusu sekta za nishati na madini katika ngazi ya shahada
za uzamili na uzamivu, suala ambalo, Balozi Mengoni aliahidi kulifanyia
kazi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia) na Balozi
wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni, wakiwa katika picha ya
pamoja, baada ya kikao baina yao.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiwa
ameshikana mikono na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni
(kushoto) na Ofisa kutoka Ubalozi huo (kulia), ikiwa ni ishara ya ushirikiano
baina ya nchi ya Italia na Tanzania.
Mtaalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Jensen
Mahavile, akifafanua jambo kuhusu fursa za uwekezaji katika miradi ya
umeme vijijini, wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni
(hawapo pichani). Wengine pichani ni viongozi na wataalam wa Wizara na
Taasisi zilizo chini yake, walioshiriki kikao hicho.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto),
akimsikiliza kwa makini Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni
(kulia), wakati wa kikao baina yao hivi karibuni. Kushoto kwa Waziri ni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...