Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
George Simbachawene ameziagiza Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kuhakikisha
kuwa fedha zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa katika Mpango wa
kunusuru kaya maskini unaofanywa kwa uratibu wa Mfuko wa Maendeleo
ya jamii (TASAF) kurejeshwa ili ziweze kuwanufaisha walengwa.
Mhe. Simbachawene pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri
kuwasimamisha kazi Waratibu wote wa TASAF wilaya ili kufanya
uchunguzi wa jinsi walivyojihusisha katika kuvuruga utekelezaji wa Mpango
wa kunusuru kaya maskini kwa kuandikisha kaya zisizokuwa na sifa na
ametaka wale wote watakaobainika kuhusika katika kutenda makosa
mamlaka za kinidhamu kuchukua hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma leo,
Mhe. Simbachawene amesema usimamizi dhaifu wa mpango wa TASAF
katika ngazi za halmashauri hususani Waratibu wa Mpango wa TASAF
Wilaya wasiokuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu yao
imesababisha fedha za Mpango wa TASAF kutumiwa na watu wasiokuwa
walengwa.
Waziri Simbachawene pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri
kuwachukulia hatua watumishi wa ngazi za Kata, Mitaa na Vijiji ambao kwa
namna moja au nyingine watabainika kuhusika katika kuvuruga Mpango wa
kuzinusuru kaya maskini kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewataka Wakuu wa Mikoa kujiridhisha
katika mikoa yao ikiwa Wakurugenzi watachukua hatua stahiki dhidi ya
watumishi wasiokuwa waaminifu na kuwataka kumpelekea taarifa hiyo
ndani ya siku kumi na nne kuanzia leo tarehe 25/11/2016.
Mheshimiwa Simbachawene ameitaja mikoa inayoongoza kwa matumizi
mabaya ya fedha za Mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na
TASAF kuwa ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, , Shinyanga,
Arusha, Kigoma, Dodoma, Arusha na Mbeya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...