Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga
akiongozana na baadhi ya wakurugenzi wa Mfuko na uongozi wa Hospitali ya Kairuki
walipotembelea maeneo mbalimbali ya hospitalini hapo kuangalia huduma zinazotolewa kwa
wanachama wa Mfuko. Pichani akimjulia hali mwanachama wa Mfuko aliyelazwa hospitalini hapo.
Na Grace Michael
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga
amezitaka Hospitali zote nchini zinazohudumia wanachama wake kuhakikisha zinatoa
huduma bora na zinazostahili kwa wanachama ikizingatiwa ukweli kwamba
wamekwishazilipia huduma hizo kabla ya kuugua.
Aidha amewahakikishia wanachama wa Mfuko kwamba, Mfuko umejipanga
kuwahudumia na kutatua kero wanazokabiliana nazo wakati wa kupata huduma ili
wajivunie huduma walizolipia.
Bw. Konga amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kujionea namna wanachama wa
Mfuko wanavyohudumiwa katika Hospitali ya Kairuki mjini Dar es Salaam ambapo mbali
na kuona huduma pia alipata fursa ya kuzungumza na wanachama waliofika hospitalini
hapo kupata huduma.
Bw. Konga akiwasikiliza wanachama wa Mfuko waliokuwa wakipata huduma za matibabu hospitalini hapo.
Akizungumza na wanachama katika Hospitali ya Kairuki, Bw. Konga alisema kuwa
ameamua kuanza ziara ya kutembelea hospitali zote ili kukutana na wanachama,
kusikiliza kero zao pamoja na kuzungumza na watoa huduma kwa lengo la kutatua
matatizo yaliyopo na kujenga uhusiano bora.
“Nimeamua kuanza rasmi ziara hizi za kikazi kuwaona moja kwa moja wanachama
wanahudumiwa ili nizungumze nao na kupata maoni kutoka kwao…wanachama kwangu
ndio kipaumbele cha kwanza kwa kuwa ndio wametupa dhamana ya kuwahudumia na
kukaa na fedha zao hivyo binafsi sitakubali kuona mwanachama akipata huduma
hafifu”. Alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa kitendo cha kutoka na kusikiliza wanachama kitasaidia kwa kiasi kikubwa
kuboresha huduma lakini pia kukutana uso kwa uso na wananchi ambao Mfuko
unawahudumia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...