Rais wa Ivory Coast,
Alassane Ouattara amesema makubaliano yamefikiwa Jumamosi (07.01.2017) kumaliza uasi wa jeshi wa siku mbili ambao ulirejesha hali ya wasi wasi wa usalama katika taifa hilo linaloongoza kwa zao la kakao duniani .
Rais Ouattara alisema hayo wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri siku ya jumamosi jioni. Hapo mapema , waziri wake wa ulinzi Alain-Richard Donwahi , aliongoza ujumbe wa majadiliano pamoja na wanajeshi hao wanaolalamika katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, Bouake, ambako uasi ulianzia Ijumaa asubuhi na kushuhudia wanajeshi wakifyatua risasi hewani.
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara |
Lakini katika ishara za mapema kwamba si kila mwanajeshi alikuwa akishiriki uasi huo, waasi mjini Bouake walianza kufyatua tena bunduki zao za Kalashnikov pamoja na silaha nyingine baada ya tangazo la Ouattara, na kusababisha Donwahi kukamatwa na kuwekwa katika nyumba ya afisa wa mji huo pamoja na ujumbe wake na waandishi habari.
Kundi hilo hatimaye liliweza kuondoka kabla ya saa kumi jioni, alisema mmoja wa mateka , Aboubakar Al Syddick, mwandishi wa habari wa gazeti la mjini Abidjan la L'Intelligent. Wizara ya ulinzi baadaye ilitoa taarifa ikikaja kwamba Donwahi alikamatwa kinyume na matakwa yake, ikisema alikuwa tu akiendelea kufanya majadiliano.
Katika tangazo lake , Rais Ouattara alisema yuko tayari kutilia maanani madai ya wanajeshi hao wanaodai fedha zaidi na mazingira mazuri katika maeneo wanayoishi pamoja na kazini, lakini alikosoa mbinu walizotumia za uasi.
"Nataka kusema kwamba njia hii ya kudai si sahihi. Kwa kweli , inachafua taswira ya nchi yetu baada ya juhudi zetu zote za maendeleo ya kiuchumi na kujijengea nafasi ya kidiplomasia," alisema.
Rais Ouattara aliingia madarakani mwaka 2011 baada ya mzozo wa baada ya uchaguzi ambao ulisababisha zaidi ya watu 3,000 kuuwawa.
Mzozo huo ulizushwa na kukataa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo kukubali kushindwa na kujiuzulu. Machafuko hayo yalifikisha kilele cha mzozo uliokuwa ukitokota wa zaidi ya muongo mmoja ambao ulianza kwa mapinduzi ya kwanza nchini humo mwaka 1999.
Mzozo huo sio mwisho wa matatizo
Rais huyo mpya anakabiliwa na changamoto nyingi katika kujaribu kujenga jeshi la pamoja. Wadadisi wa masuala ya kisiasa walitabiri serikali itatoa fedha ili kuzima mzozo wa wiki hii, kama ilivyofanya wakati wanajeshi walipofanya uasi kama huo mwaka 2014.
Maelezo kuhusiana na makubaliano hayo hayakupatikana mara moja. Licha ya juhudi hizo za serikali kupata suluhisho la haraka, tukio hilo linaelekeza katika matatizo yanayoendelea kuwapo katika nchi ya Ivory Coast inayojitoa kutoka katika matatizo, amesema Cynthia Ohayon, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afrika magharibi kwa ajili ya kundi la kimataifa linaloangalia mizozo.
"Hii ni tukio jingine linalokumbusha kwamba masuala ambayo bado yapo ambayo yalisababisha mzozo bado hayajatatuliwa," amesema. "Baadhi ya watu wanasahau na wanafikiri kwamba kila kitu kinakwenda vizuri nchini Cote d'Ivoire. Nafikiri hali hii inapaswa kupunguzwa."
Imeandikwa na Mtandao wa DW
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...