Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa agizo kwa
wasanii wa hapa nchini kutumia lugha fasaha ya Kiswahili katika kazi zao ili
kuitangaza lugha hiyo inayotambulisha Taifa letu.
Agizo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizindua program ya
kuuza muziki na filamu kwa njia ya mtandao iliyoandaliwa na Kampuni ya
Afroprimiere.
Prof. Gabriel alisema kuwa Tanzania inatambulika Duniani kwa lugha ya Kiswahili
hivyo wasanii wana nafasi kubwa ya kuendelea kutumia lugha hiyo kwa ufasaha katika
kazi zao wanazofanya ili kukuza lugha ya Kiswahili.
“Wasanii mnafanya kazi zenu kwa Kiswahili ni vyema mkatumia lugha hii kwa ufasaha
zaidi lakini pia kuweni sehemu ya mafanikio ya mpango huu ili mfanikiwe zaidi.”
Alisema Prof. Elisante.
Aidha amewahakikishia wasanii kuwa Serikali itaendelea kutunza haki za wasanii na
kuwaunga mkono katika programu hii ili iwe na faida kwa Serikali katika kupata
mapato na wasanii pia kupata faida ya kazi zao.
“Kutunza Kazi za wasanii ni jukumu letu, nawahakikishia hakuna atakayekosa faida
katika jambo hili kama tutakua pamoja na kushirikiana.” Aliongeza Prof Gabriel.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Afroprimiere ambao ndio
waandaaji wa program hiyo Bw. Fredy Ngimba amesema kuwa program yao inalenga
kuwasaidia wasanii namna wanavyoweza kufaidika na biashara ya kazi zao
mtandaoni.
“Programu hii itawasaidia wasanii kujua idadi kamili ya wanunuzi wa kazi zao
mtandaoni na namna ambavyo watagawanya mapato kwa wote wanaohusika kuanzia
Serikali, Waandaji, Watengenezaji na wasambazaji wa kazi hizo.”Alisema Bw.
Ngimba.
Mapato kwa wote wanaohusika katika kazi hiyo yanaonyesha kuwa Msanii ambaye ndio
mwenye kazi yake atapata 50%, Muandaaji 25%, Kampuni ya Mawasiliano 20%,
mtengenezaji 08% na Serikali 18%.imeandikwa na Shamimu Nyaki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Pof.Elisante Ole
Gabriel akizungumza na Wasanii (hawapo pichani ) katika uzinduzi wa programu ya
kuuza muziki na filamu kupitia mtandao (online)iliyoandaliwa na Kampuni ya
Afroprimiere jana Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi maendeleo ya
Sanaa Hajjat Shani Kitogo na wa kwanza Kulia ni Bw.Fredy Ngimba Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni hiyo.
Baadhi ya Wasanii walioshiriki katika uzinduzi wa programu ya kuuza muziki na
filamu kupitia mtandao (online) iliyoandaliwa na Kampuni ya Afroprimiere jana Jijini
Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...