Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wameihakikishia Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB) kuwa wamejizatiti kikamilifu kwenda kusaidia juhudi kubwa
za Bodi hiyo katika kuitangaza Tanzania kama eneo bora la Utalii duniani katika
nchi wanazokwenda kufanyakazi sambamba na kuhamasisha wafanyabiashara kutoka
mataifa hayo kuwekeza nchini katika sekta ya utalii ikiwa ni utekelezaji wa
jukumu lao kubwa la kukuza diplomasia ya uchumi.
Wamepongeza juhudi zinazofanywa na TTB katika kuvitangaza
vivutio vyetu vya utalii lakini wakaomba iangalie namna gani inaweza kusaidia
katika kuboresha huduma zitolewazo na wadau wa utalii kwa watalii wanaotembelea
Tanzania kama vile mahotelini kwani bado hatufanyi vema katika suala la huduma
bora na nzuri kwa watalii. Aidha wameiomba TTB kushauri mamlaka na watoa huduma
wengine katika sekta ya utalii kupunguza gharama wanazotoza kwani ni kubwa sana
kiasi cha kuifanya Tanzania kulalamikiwa na wageni wengi kuwa ni eneo la utalii
ghali sana ukilinganisha na nchi nyingine ambazo ni washindani wetu katika
sekta ya Utalii.
Hayo yamesemwa leo na
mabalozi hao wakiongozwa na Balozi Omari Yusuph Mzee walipotembelea makao makuu
ya Bodi ya Utalii Tanzania kwa lengo la kuzungumza na Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Bodi hiyo Bi Devota Mdachi na kupanga mikakati ya namna balozi hizo zinavyoweza
kushirikiana na TTB katika kuitangaza Tanzania na kuhamashisha wawekezaji
kutoka nchi wanazokwenda kufanyakazi kuja nchini kuwekeza katika sekta ya
utalii.
Mapema Mkurugenzi
Mwendeshaji wa TTB Bi Devota Mdachi aliwaelezea waheshimiwa mabalozi mikakati
mbalimbali ambayo Bodi yake imekuwa ikitekeleza katika kuitangaza Tanzania nje
ya nchi kwa lengo kuvutia watalii wengi zaidi na kukuza utalii kwa ujumla.
Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuweka matangazo katika
maeneo na vyombo mbalimbali vya habari nje ya nchi, kualika na kuleta nchini
watu maarufu ili kuja kutembelea vivutio vyetu vya utalii, kuteua mabalozi wa
hiari wa utalii na kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Mkurugenzi Mwendeshaji Bibi Devota Mdachi aliwakabishi
mabalozi hao vielelezo mbalimbali vya utalii wa Tanzania na kuahidi kuwa bodi
yake itakuwa ikiwatumia vielelezo mbalimbali vya utalii vitakavyo wasaidia
katika kutekeleza jukumu la kusaidia utangazaji utalii katika nchi walizopangiwa.
Mabalozi hao watano na nchi wanazo kwenda ni Omari Yusuph Mzee (Algeria),
Matilda Masuka (Korea Kusini), Dkt. Pindi Chana (Kenya), Grace Mgovano
(Uganda), Fatma Rajab (Qatar) na Balozi Abdallah Kilima (Oman).
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa TTB Bi devota Mdachi akizungumza na Mabalozi waliomtembelea
ofisini kwake jana.Kushoto ni Balozi Omari Yusuph Mzee na kulia ni Balozi
Abdallah Kilima.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt Pindi Chana akisisitiza jambao wakati wa
mazungumzo baina yao na Mkurugenzi Mwendshaji wa TTB walipomtembelea ofisini
kwake Dar es salaam.
Mkurugenzi
Mwendshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi (kulia) akimkabidhi
Balozi Abdallah Kilima moja ya majarida ya TTB yanayozungumzia utalii wa
Tanzania wakati timu ya mabalozi sita walioteuliwa hivi karibuni walipomtembela
Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Mabalozi
wanaowakilisha Tanzania katika baadhi ya nchi duniani wakiwai katika picha ya pamoja
na Mkurugenzi wa TTB Bi Devota Mdachi (wa nne kushoto) na baadhi ya Maafisa
waandamizi wa TTB . Kutoka kushoto
ni Bw. Geofrey Meena Meneja Masoko wa TTB, Mh. Balozi dkt Pindi Chana , Mh.
Balozi Omari Yusuph Mzee, Mh. Balozi Fatma Rajab (wa tano), Mh. Balozi Grace Mgovano (wa
sita), Mh. Balozi Matilda Masuka (wa saba) na Bw. Philip Chitaunga Meneja
Huduma kwa watalii wa TTB.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...