THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

UJERUMANI YAIOMBA TANZANIA KUIUNGA MKONO KATIKA UCHAGUZI WA NAFASI YA MJUMBE WA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA.


Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga amefanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Balozi Harro Adt, ambapo alipokea, niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ujumbe maalum kutoka kwa Kansela Markel.

Akizungumzia ziara ya Balozi Adt nchini, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa "Kansela Merkel amemtuma Balozi Adt, kuleta ujumbe maalum ambao ni ombi kwa Rais Magufuli la kuisaidia Ujerumani katika kugombea nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi wa nafasi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018".

Balozi Dk. Mahiga alieleza kuwa dhamira ya Ujerumani ya kugombea nafasi hiyo ni kusaidia mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kuridhia nchi za Afrika katika mchakato wa kupokea nafasi mbili za kudumu katika baraza hilo. Nchi nyingine zinazogombea nafasi hizo ni Israel na Ubelgiji.

Balozi Mahiga alisema kuwa, Ujerumani imeahidi masuala kadhaa kama vile kusimamia amani katika jumuiya ya kimataifa na katika ukanda wa Afrika, kusimamia haki za binadamu katika ngazi ya dunia na kuendelea kuimarisha uhusiano wake na nchi nyingine.

Aidha, Ujerumani imesisitiza nia yake ya kuunga mkono mageuzi mapya katika bara la Afrika ambayo yataikomboa Afrika na kuleta maendeleo zaidi barani humu.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa ameiomba Ujerumani isaidie ujenzi wa jengo mahususi la mahakama ya Afrika iliyopo mjini Arusha ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo mzima wa mahakama barani Afrika pamoja na kuisaidia Afrika katika kupambana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, mjumbe maalum kutoka Ujerumani Balozi Adt, alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata alipowasili nchini.

Aidha, Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujenrumani alieleza matumaini yake kuwa Tanzania ambayo ni rafiki wa Ujerumani kihistoria itatoa msaada juu ya nafasi hiyo ili kusaidia kutekeleza malengo waliojiwekea kiufanisi kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uhusiano kati Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria na wakati wote nchi mbili hizo zimekuwa zikifanya kila jitihada za kuuimarisha.

Chini ya uhusiano huo, Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile elimu, miundombinu na wanyamapori.