Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amewataka wazazi kuacha tabia ya kuiachia Serikali na mashirika binafsi kuwawezesha vijana na badala yake washiriki kuwasaidia vijana hao ili waweze kujitegemea.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya Serikali katika kusaidia maendeleo ya vijana waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International.

Ndemanga amesema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwa vijana katika eneo hilo kwani wamefundishwa sio tu mafunzo ya ufundi bali pia ujasiriamali, namna ya kuweka hisa, kujiwekea fedha kwa ajili ya matumizi ya baadaye pamoja na masuala ya kodi lakini tatizo linalojitokeza ni wazazi kuwaachia Serikali na wadau wengine kushughulikia kila kitu.

“Changamoto ni nyingi katika kusaidia vijana hasa ambao tayari walishapata mafunzo kwa sababu wazazi wakishafahamu kuwa vijana wao wako chini ya mradi basi wanawaachia mzigo wote Serikali na wadau mbali mbali hivyo nawasihi wazazi wawasaidie vijana wao katika kujitafutia ajira”.alisema Ndemanga.

Ametoa rai kwa vijana kujitokeza kwa wakati pindi miradi hiyo inapotokea kwa sababu wengi wao wamekuwa wakichelewesha kuleta maombi hayo mpaka muda wa mafunzo unafika hivyo kwa kuwa mafunzo hayo hufanyika kwa muda maalum, vijana wanatakiwa wajitokeze mapema kwa idadi kubwa.

Aidha, Ndemanga amewataka vijana waliopata mafunzo kuwafundisha wenzao na pia wanaojiajiri wakumbuke kuwaajiri vijana wengine ili kupunguza mrundikano wa vijana wanaozagaa mitaani bila kuwa na kazi za halali.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hamida Mohamed amekabidhi cherehani mbili kwa vijana wawili waliomaliza mafunzo ya ufundi chini ya mradi huo ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha ushiriki wa wazazi katika kuwakomboa vijana hasa kwenye masuala ya kiuchumi.

“Mradi huu umetusaidia sana kuwaona vijana wenye mazingira magumu hasa walemavu na kufahamu matatizo yao hivyo kutufanya sisi viongozi wa Serikali kufahamu namna ya kuwasaidia huku tukisaidiana na wadau mbalimbali”, alisema Mhe. Hamida.

Mradi huo wa miaka mitatu 2015 hadi 2018 unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...