Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven ya mkoani Arusha, walioachishwa kazi mwaka 2000, wameshalipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria na taratibu hivyo hawastahili kudai malipo yoyote ya nyongeza.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maaluum (CCM) Arusha, Mhe. Catherine Magige aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo.

Mhe. Magige aliliambia Bunge kuwa waliokuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo ambao waliachishwa kazi mwaka 2000, hawajalipwa mafao yao hadi sasa.

Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa katika zoezi la ulipaji wa mafao kwa wafanyakazi hao Serikali ililipa Sh. 217,366,296 mwezi Januari, 2000 ambapo baadae walipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao kuwa wamepunjwa.

“Serikali baada ya kupokea malalamiko hayo, ilihakiki na baada ya kujiridhisha mwezi Agosti, 2000, ilitoa idhini ya kulipa tena kiasi cha Sh. 273, 816, 703 kwa ajili ya mapunjo ya mishahara na mafao ya wafanyakazi hao” aliongeza.

Hata hivyo, Mhe. Magige hakuridhishwa na majibu ya Dkt. Kijaji na alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza alisema kuwa Serikali imewalipa wafanyakazi hao awamu ya kwanza tu na hawakupewa nyongeza yoyote licha ya kuwasilisha malalamiko hayo.

Mhe. Magige aliongeza kuwa Wizara ya Fedha ilishawahi kwenda kufanya uhakiki na kubaini kuwa kulikuwa na mapungufu, na Serikali iliipa jukumu la kusimamia malipo hayo Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo mpaka sasa bado haijalipa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii (MB), Mhe. Ramo Makani aliliomba Bunge limpe muda wa kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu ili aweze kutoa majibu sahihi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...