Na Husna Saidi na Nuru Juma- MAELEZO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Trilioni 10.87 mpaka kufikia Machi mwaka huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Edward Kichere wakati wa mahojiano na mtangazaji wa TBC1 Rashid Salum katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa kila siku za Jumatatu saa moja kamili jioni na Alhamisi saa tatu na nusu usiku.

Kichere alisema, mwaka huu wa fedha 2016/2017 TRA inatakiwa kukusanya Trilioni 15.105 na hadi kufikia Machi mwaka huu TRA imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 10.87.

Aliendelea kwa kusema kuwa mpaka kufikia Juni mwaka huu TRA itahakikisha inatimiza lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 15.105 ili kusaidia Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Alisema kuwa TRA ina waajiriwa wapya ambao wamepewa mafuzo ya miezi sita katika chuo cha kodi juu ya mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi ambao waliajiriwa moja kwa moja na mamlaka hiyo kwaajili ya kutekeleza majukumu ya ukusanyaji kodi ndani ya nchi.

“Tunatumia mfumo wa Tehama kukusanya kodi na mifumo mingine mbalimbasli kama vile Tigo Pesa , Airtel Money na MPesa ili kurahisishia watu kulipa kodi wakiwa nyumbani na kuepuka usumbufu,” alisema Kichere.

Kichere aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha mapato yameongezeka mpaka kufikia asilimia 9.9 hadi 10 licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo hawakuweza kukusanya.

Aidha Kichere alisema Mamlaka kwa sasa imejipanga kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi stahiki na kwa mujibu wa sheria bila kutumia nguvu au uonevu wowote.

Hata hivyo mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa walipa kodi kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kutoa semina kwa watumishi wa umma , kuandaa makongamano ambayo yanatoa elimu, kupitia mitandao ya kijamii na ziara mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata elimu pamoja na kujua wajibu wao katika kulipa kodi ili kuleat maendeleo nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...