Na Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa wito kwa wataalam nchini, hususan walioko katika sekta za mafuta na gesi kulisaidia Taifa kuepukana na mikataba mibovu kwa kutumia utaalam wao badala ya wao kuendelea kulalamika kama wananchi wa kawaida.

Profesa Muhongo alitoa wito huo jana, Aprili 27, 2017 wakati akizindua Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo, Profesa Muhongo alisema kwamba, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu Taifa kuibiwa rasilimali mbalimbali na makampuni ya kigeni kutokana na mikataba mibovu iliyoingiwa awali.

“Ni kwa sababu hiyo, uteuzi wa wajumbe wa Bodi hii ya PURA, umezingatia sifa za hali ya juu za kitaaluma mlizonazo, ili pamoja na mambo mengine muweze kulisaidia Taifa kunufaika ipasavyo na rasilimali hizi adhimu za mafuta na gesi, kwa kuhakikisha mikataba inayoingiwa, inakuwa yenye manufaa kwetu.”

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Bodi ya PURA ina wajumbe watano ambao wamebobea katika taaluma za sheria, fedha, uhasibu na mazingira; sifa ambazo zinaifanya Bodi hiyo kuwa miongoni mwa Bodi bora kabisa hapa nchini.

Aliwataka wataalam hao kuachana na kasumba ya kulalamika kuwa Taifa linaibiwa badala yake watumie utaalam na ubobezi wao kuhakikisha changamoto hiyo inabaki kuwa historia nchini hususan katika sekta wanayoisimamia.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisisitiza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) iliyofanyika Aprili 27, 2017 makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Habass Ng’ulilapi (kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe), akiwasomea majukumu yao, wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) iliyofanyika Aprili 27, 2017 makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiwakabidhi vitendea kazi baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), mara baada ya kuizindua rasmi katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...