Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Said Rajabu Said (36), kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na mafuta ya Simba.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri, baada ya kumaliza ushahidi kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashtaka na washtakiwa kujitetea.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo kinyume na kifungu 86(1)(2)(c)(ii) ya sheria ya wanyama pori namba 5 ya 2009.

Akisoma hukumu Hiyo Hakimu Mashauri amesema kuwa upande wa mashtaka wamethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa Said ametenda kosa hilo.

Kabla hajamsomea mshtakiwa adhabu yake, Mashauri aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ambapo wakili wa Serikali, Adolf Mkini aliomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia na nia ya kutenda makosa kama hayo.

"Mheshimiwa hakimu, sina kumbukumbu za makosa ya nyuma kwa mshtakiwa, ila naomba mahakama yako tukufu itoe adhabu Kali kwa mshtakiwa na kwa wengine kwenye nia ya kuharibu maliasili za nchi", amesema Mkini.

Kwa upande wa mshtakiwa Said katika utetezi wake ameiomba mahakama imuachie huru kwa sababu ana watoto watano na familia inayomtegemea na yeye ndio kila kitu kwenye familia hiyo.

" Nimezingatia yote yaliyosemwa na upande wa mashtaka na utetezi wa shahidi, nchi hii ina sheria zake za kulinda maliasili hivyo, Mahakama inakuhukumu kwenda jela miaka ishirini ile iwe fundisho kwako na kwa wengine wenye tabia kama yako".

Mshtakiwa anadaiwa kuwa, Februari 8,2016 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, alikamatwa akiwa na mafuta ya Simba yenye thamani ya Sh 10,711,400 bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa wanyama pori.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...