Na Benedict Liwenga-WHUSM.

Halmashauri nchini zimetakiwa kuitikia wito wa kununua dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria zilizoanza kuzalishwa hapa nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria cha Tanzania Biotech Products Limited kilichopo Kibaha Mkoani Pwani, Bw. Samwel Mziray wakati alipokutana na Waandishi wa habari na kufanya nao mazungumzo juu ya shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho.

Bw. Mziray amesema kuwa, dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria zinapaswa kununuliwa na kila Halmashauri nchini kwa maagizo yaliyotolewa na Serikali kupitia waraka wake kwa kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kilijengwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali katika kupambana na malaria nchini. 

Hata hivyo amebainisha kwamba mpaka sasa mwitikio wa halmashauri umekua mdogo kwani ni halmashauri mbili tu za Geita pamoja na Mbogwe ndizo zimeshanunua dawa hizo.

“Lengo la Serikali kuja na mpango huu ni kupunguza vifo vitokanavyo na malaria nchini na kupunguza gharama kubwa ya kununua dawa na vifaa tiba vya kupambana na malaria”, alisema Mziray.

Amesema kwamba iwapo kama halmashauri zitanunua dawa hizo na kuzitumia, ugonjwa huo utapungua kwa kiasi kikubwa nchini na hivyo serikali kuelekeza fedha zake katika shughuli za maendeleo.

Amesema kwamba, kwa Afrika kiwanda hicho ni moja ya kiwanda kilichobahatika kujengwa Tanzania ambapo nia ya Serikali ni kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa kuharibu mazalia ya mbu.
Jengo la Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria lililozinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn tarehe 2 Julai, 2015 Kibaha, Pwani.
Mtaalam wa Maabara ya Uandaaji Bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Bw. Fumbuka Pauline akiwaeleza Waandishi wa habari baadhi ya kazi wazifanyazo wakati wa kuwaandaa bakteria 15 Mei, 2017. Kushoto ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Bw. Samwel Mziray.
Mmoja wa Waandishi wa Habari (kulia) akipiga picha ya bakteria wanaoonekana kwa kifaa maalum cha kuangalia bakteria (Microscope) katika Maabara ya kuaandaa bakteria 15 Mei, 2017 Kibaha, Mkoani Pwani.
Mtaalam wa Maabara ya Uandaaji bakteria katika Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu wa Malaria kilichopo Kibaha Mkoani akiangalia bakteria kwa kutumia kifaa maalum (Microscope) kabla ya kuwapeleka sehemu inayohusika kwa ajili ya hatua nyingine, 15 Mei, 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...