Balozi wa Tanzania ndani ya
Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba tarehe 15 Mei
alikabidhi hati zake za uwakilishi kwenda kwa Mhe. Azali Assoumani, Rais wa
Muungano wa Visiwa vya Komoro. Hafla ya kukabidhi hati hizo ilifanyika kwenye
Ukumbi wa Ikulu ya Komoro ijulikanayo kama
Beit. Wakati akisoma risala yake, Mhe. Balozi alijitambulisha kwa Mhe.
Rais na kueleza furaha yake ya kuteuliwa kwake kuwa Balozi wa pili kutoka
Tanzania kuja kutumikia nchini Komoro. Aidha, Mhe. Balozi alieleza furaha yake
kwa mapokezi mazuri aliyopatiwa tangu kuwasili kwake Visiwani Komoro ambapo aliongezea kwa kueleza kuwa
anajisikia yupo nyumbani.
Alieleza kuwa anatambua kazi
kubwa iliyopo mbele yake na kuahidi kuwa katika kipindi chake wakati akiwa
Balozi nchini hapa atajitahidi kukuza mahusiano yaliyopo baina ya Tanzania na
Komoro. Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alieleza dhamira yake ya kutaka kuona
mahusiano baina ya nchi hizi mbili yanakuwa na manufaa kwa pande zote
halikadhalika kukua kwa uhusiano wa kindugu kwani mahusiano baina ya Tanzania
na Komoro ni ya kihistoria.
Akijibu risala hiyo, Mhe. Azali Assoumani, Rais
wa Muungano wa Visiwa vya Komoro naye alianza kwa kuonyesha furaha yake ya
kuwasili kwa Balozi pamoja na kukiri kupokea barua ya kurejea Balozi aliyepita
na kuwasili kwa Balozi wa sasa. Alieleza kuwa kila Mkomoro hujisikia nyumbani
pindi anapo tembelea Tanzania kutokana na ukarimu wanao onyeshwa wanapokuwa
huko. Aidha Mhe. Rais alimuhakikishia Mhe. Balozi kuwa atarajie kupata
ushirikiano wake pamoja na wa Serikali yake katika kipindi chote atakapo kuwa
hapa.
Mhe. Balozi Mabumba alichukua
fursa hiyo pia ya kumuomba Mhe. Rais Azali afanye ziara ya kikazi nchini
Tanzania ili kuweza kudumisha mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili.
Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba akiwasili kwenye Ikulu ya Komoro ijulikanayo kama Beit tayari kwa kukabidhi hati zake za uwakilishi kwa Mhe. Azali Assoumani, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Komoro.
Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba akisoma risala yake kwenye Ikulu ya Komoro ijulikanayo kama Beit kabla ya kukabidhi hati zake za uwakilishi kwa Mhe. Azali Assoumani, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Komoro.
Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba akikabidhi hati zake za uwakilishi kwa Mhe. Azali Assoumani, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Komoro kwenye Ikulu ya nchi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...