Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Mgogoro wa Libya ameendelea na juhudi zake za usuluhishi wa mgogoro wa Libya kwa kushiriki katika Kikao cha 11 cha Mawaziri wa Nchi Jirani na Libya kilichofanyika jijini Algiers, Algeria tarehe 8 Mei, 2017.

Katika Kikao hicho, Rais Mstaafu amepongeza juhudi zinazoendelea za kupatanisha pande zinazogombana nchini Libya na mafanikio yanayopatikana ikiwemo kuimarika kwa hali ya usalama, kudhibitiwa kwa vitendo vya kigaidi, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji wa mafuta na kufufuliwa kwa mawasiliano kati ya pande zinazohasimiana.
 
 Ameunga mkono jitihada zinazochukuliwa na nchi za Algeria, Misri, Tunisia na UAE katika kuhimiza mazungumzo ya Amani. Amesisitiza umuhimu wa pande mbili za mgogoro kuheshimu Makubaliano ya Amani ya Libya (Libya Political Agreement) na kutekeleza vipengele vyake bila ajizi.

Akiwa jijini Algiers, Rais Mstaafu amefanya pia mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo anayemuwakilisha Mwenyekiti wa Kamati wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kuhusu Libya Mhe Jean-Claude Gakosso na Balozi Martin Kobler, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Mgogoro wa Libya (UNSMIL).

Rais Mstaafu anatarajiwa kumalizia ziara yake nchini Libya kukutana na viongozi wakuu wa pande zinazotofautiana nchini humo.
Rais Mstaaafu Dkt Jakaya Kikwete akifuatilia Mkutano wa Nchi Majirani wa Libya
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Mgogoro wa Libya Balozi Martin Kobler jijini Algiers
Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akitoa msimamo wa Umoja wa Afrika kuhusu Mgogoro wa Libya .

Rais Mstaafu katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo na Mwenyekiti wa AU Mhe. Jean-Claude Gakosso. Kushoto ni Mkuu wa Ofisi ya Uwakilishi wa AU kwa Libya Bi. Wahida Ayari 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...