CHEMBA ya Madini na Nishati (TCME) imetambua na kuguswa na taarifa zisizo sahihi kwamba kampuni zinazojihusisha na uchimbaji mkubwa wa madini zimekuwa zikifanya shughuli zake hapa nchini bila ya kulipa kodi ya mapato. 

Chemba hii ni muwakilishi wa makampuni wanachama waliorasimisha shughuli zao katika sekta ya madini kuanzia kampuni ndogo za utafiti wa madini hadi wachimbaji wakubwa na wa kati wa madini, pamoja na makampuni yanayotoa huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti na uchimbaji wa madini.

Chemba na wanachama wake wanaunga mkono uwepo wa sekta ya uchimbaji madini inayoratibiwa vema na inaweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha shughuli za wanachama wake zinaendeshwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na mamlaka za Serikali hapa nchini.

Makampuni ya uchimbaji madini hapa nchini yanaratibiwa kwa kiwango cha juu na mamlaka zilizo chini ya Serikali ili kuhakikisha yanafanya shughuli zake kwa kufuata sheria na kanuni za nchi. Makampuni haya yameendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa njia mbali ikiwemo utengenezaji wa ajira pamoja na ulipaji wa kodi.

Katika ripoti ya utendaji ya mwaka 2015 ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini. Tanzania (TMAA) ambao wanafanya kazi chini ya Wizara ya Nishati na Madini, imeripotiwa kwamba makampuni makubwa ya uchimbaji madini hapa nchini, kwa ujumla wake, kati ya mwaka 2009 na 2015 yameweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 870 (USD390 Milioni) kama mrabaha, na zaidi ya Shilingi Bilioni 680 (USD305 Milioni) kama kodi ya mapato, hii ni mbali na kodi nyingine zisizo za moja kwa moja ambazo pia zimelipwa.

Katika mwaka wa 2015 pekee, migodi mitano mikubwa ya uchimbaji Dhahabu pamoja na mgodi mmoja wa kuchimba Almasi, kwa pamoja iliweza kulipa zaidi ya Shilingi Bilioni 146 (USD65.5 Milioni) kama mrabaha na zaidi ya Shilingi Bilioni 380 (USD170 Milioni) kama kodi nyingine ikiwamo kodi ya mapato. Viwango hivi ni dhahiri vitakuwa vimeongezeka zaidi kwa mwaka 2016.

Zimekuwepo pia taarifa kwamba makampuni haya ya uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa yakifaidika kwa kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pasipo uhalali wa kupata marejesho hayo. Taarifa hizi si sahihi. Ukweli ni kwamba makampuni ya uchimbaji mkubwa wa madini yamekuwa na yataendelea kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kuuza madini yote ambayo wanayazalisha hapa nchini. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 (VAT ACT 2014) wafanyabiashara ambao mauzo yao yote hufanyika nje ya nchi hukadiriwa kodi ya ongezeko la thamani kwa kiwango cha sifuri (zero rated) na kwa sababu hiyo basi hustahili kurejeshewa kodi ya VAT ambayo huilipa kupitia manunuzi anayoyafanya hapa nchini.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...