Na Fatma Salum (MAELEZO)

Serikali imewataka Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kote nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ili kuleta ufanisi katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu kwenye Utumishi wa Umma.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw.Nyakimura Muhoji wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Muhoji alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Tume hiyo imefanya ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Taasisi 41 na kubaini kwamba kuna baadhi ya Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu hazitekelezi ipasavyo majukumu yao hususan katika usimamizi wa masuala ya ajira na nidhamu hivyo kupunguza ufanisi katika utendaji kazi.

“Ukaguzi wa Rasilimali Watu umefanyika katika Taasisi 41 ambazo ni Sekretariet za Mikoa mitano ikiwemo Morogoro, Iringa, Mbeya, Arusha na Mwanza, Mamlaka za Serikali za Mitaa 30 zilizopo kwenye mikoa hiyo pamoja na Wakala na Taasisi 6 kwa lengo la kuangalia ni kiasi gani Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma.” alieleza Muhoji.

Naye Katibu Msaidizi Idara ya Afya kutoka Tume hiyo Bw. Peleleja Masesa alisema kuwa hali ya uwasilishaji wa taarifa zinazohusu usimamizi wa Rasilimali Watu hairidhishi kwa kuwa zipo baadhi ya Taasisi za Umma hazitekelezi jukumu hilo la kisheria.

“Nasisitiza kuwa uwasilishaji wa taarifa kwa Tume ni jukumu la kisheria hivyo Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu ambao hawajawasilisha taarifa hizo wanakumbushwa kuziwasilisha kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa.” alisisitiza Masesa.

Aidha Masesa alieleza kuwa Tume hiyo pia ina jukumu la kupokea na kushughulikia Rufaa na malalamiko yanayohusu masuala ya kiutumishi kutoka kwa Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na jinsi masuala yao ya kiutumishi yalivyoshughulikiwa na mamlaka zao.

Pia alitoa wito kwa Watumishi wa Umma na Watendaji wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili ya Utumishi wa Umma na taaluma zao ili Utumishi wa Umma ukidhi matarajio ya wananchi.
Katibu Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nyakimura Muhoji akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu majukumu mbalimbali yaliyotekelezwa na Tume hiyo katika mwaka wa fedha 2016/17 kwa ajili ya kuboresha utendaji katika utumishi wa umma. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. Peleleja Masesa.
Katibu Msaidizi Idara ya Afya kutoka Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Peleleja Masesa akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 inayoelezea majukumu ya Tume hiyo. Kulia ni Katibu Msaidizi Idara ya Utumishi Serikalini kutoka Tume hiyo Bw. John Mbisso.
Katibu Msaidizi Idara ya Utumishi Serikalini kutoka Ofisi ya RaisTume ya Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taratibu za kupokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma katika Tume hiyo. Kulia ni Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. Peleleja Masesa.(PICHA ZOTE NA FATMA SALUM- MAELEZO)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...