AKINAMAMA wanaojishughulisha na kilimo cha nyanya, spinachi, kabichi na mapapai kutoka Kinyerezi jijini Dar es Salaam wameamua kujifunza pia kilimo cha uyoga kutoka kwa wenzao wa Bunju ikiwa ni hatua ya kuongeza fursa ya ujasiriamali pamoja na kubadilishana uzoefu.

Wakiongozwa na Dkt. Sophia Mlote, akinamama hao wa kikundi cha Kinyerezi Green Voice wameamua kuchukua hatua hiyo katika awamu ya pili ya kutekeleza Mradi wa Green Voices unaolenga kuwawezesha wanawake kujihusisha na shughuli za kiuchumi zinazoendana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.

Ziara hiyo ya mafunzo ya siku moja ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwahusisha akinamama 13 wa kikundi hicho cha Kinyerezi ambao wanashiriki kilimo hai katika maeneo yao kwa kutumia mabanda maalum ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita wameweza kunufaika na bidhaa wanazozalisha.

Awamu ya pili ya mradi huo wa Green Voices imeanza mwezi Aprili 2017 na itaishia Aprili 2018, ambapo mradi huo unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Dkt. Mlote alisema kwamba, wameamua kwenda kujifunza kilimo chau yoga siyo tu katika kubadilishana uzoefu, bali pia kuongeza ujuzi ili kupata tija katika shughuli za kilimo rafiki wa mazingira katika utekelezaji wa mradi huo wa Green Voices.

“Tunataka kujifunza aina mbalimbali za kilimo kwa sababu hii ni fursa nzuri ya kumwezesha mwanamke kujiajiri na kuongeza pato kiuchumi,” alisema Dkt. Mlote.

Dkt. Mlote, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo, alisema mazingira walioyonayo katika kuendesha kilimo hifadhi cha nyanya, kabichi na mapapai huko Kinyerezi hhayana tofauti na mazingira ya kilimo cha uyoga kwani shughuli zote zinafanyika katika maeneo madogo ya nyumba zao huku wakihitaji kiasi kidogo cha maji.

Mafunzo kwa vitendo. Akinamama wa Kinyerezi Green Voices wakiweka udongo kwenye mifuko kama maandalizi ya kilimo cha uyoga.

Mafunzo ya nadharia: Mkufunzi wa kilimo chau yoga wa kikundi cha Bunju Tunza Women, Bi. Esther Chiombola, akitoa mafunzo kwa wanakikundi wa Kinyerezi Green Voices waliotembelea mradi wa akinamama wa Bunju kwa nia ya kubadilishana uzoefu. 
Mshiriki kiongozi wa kikundi cha akinamama walima uyoga Bunju, Bi. Magdalena Bukuku, akimkabidhi Dkt. Sophia Mlote kitabu cha namna ya kulima uyoga.

Mkufunzi wa kilimo chau yoga, Bi. Esther Chiombola, akiwapatia vipeperushi washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja. 
Akinamama wa kikundi cha Kinyerezi Green Voices wakipita kwenye banda (shamba) la uyoga walipokwenda hivi karibuni kwa mafunzo ya siku moja ya kubadilishana uzoefu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...