Na Christina R. Mwangosi, MOHA 

Jeshi la Magereza nchini ni moja kati ya Majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yenye jukumu kubwa la msingi la kuwarekebishwa wafungwa wanaohukumiwa kwa makosa mbalimbali hapa nchini. 

Katika taratibu za Urekebishaji wa wafungwa zipo stadi mbalimbali za kilimo, ufundi na uzalishaji ambazo zinatumika  kuwarekebisha  wafungwa ili hata pale wanapomaliza vifungo vyao na kurudi uraiani waweze kutumia ujuzi walioupata katika shughuli za uzalishaji na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi lakini kuchangia pia katika maendeleo ya nchi yetu.
 Mbali na jukumu hilo la msingi la Jeshi hilo, pia Jeshi hili limekuwa likijishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula kwa wafungwa, utengenezaji wa samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisi na nyumbani, pamoja na utengenezaji wa viatu shughuli zinazofanyika katika Magereza yaliyopo hapa nchini.

Aidha Jeshi la Magereza nchini lina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza   kuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu na hivyo kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ardhi nyingi yenye rutuba inayofaa kutumika kwa kushughuli za kilimo na matumizi mengineyo ya uzalishaji vikiwemo viwanda.

Kwa muda mrefu sasa jeshi la Magereza limekuwa likitumia kiwanda chake cha Utengenezaji wa Samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Ofisi na hata nyumbani kilichopo katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
 Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza ambaye ndiye Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Ukonga cha Jeshi la Magereza nchini kilichopo jijini Dar es Salaam John Itambu anasema  kwa sasa kiwanda hicho kinafanya shughuli kubwa za aina mbili  ikwemo utengenezaji  wa samani mbalimbali  kwa ajili ya matumizi ya ofisini na nyumbani ikiwemo utengenezaji wa meza, viti, makabati,  vitanda,  meza za chakula na za ofisi,  pamoja na meza za chumbani maarufu kama ‘dressing table’.

Kamishna Msaidizi Itambu anasema kiwanda hicho kinatengeneza samani hizo  kwa kutumia mbao za kawaida zile za asili zenye ubora wa kiwango cha juu na zile za henzerani yaani miti ya  minazi ambazo nazo pia zina mvuto wa hali ya juu pia ikiwemo ubora pia. 

Anasema pamoja na utengenezaji wa samani kiwanda hicho pia kimekuwa kikijishughulisha na utengenezaji wa kazi za mikono ikiwemo mazulia, vikapu, ‘table mates’ pamoja na mazulia ya milangoni.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Itambu ambaye ndiye msimamizi wa shughuli za Kiwanda hicho anasema pamoja na kwamba Kiwanda cha Samani cha Magereza Ukonga kimekuwa kikitengeneza samani zenye ubora wa hali ya juu lakini siku zilizopita kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa ‘Oda’  ilikuwa mteja akiagiza samani za aina fulani inachukua muda mrefu kukamilishiwa mahitaji yake wakati mwingine na ubora unakuwa umepunguwa si kwa ubora aliokuwa ameuona kwenye shughuli za Maonyesho ya Sabasaba.

Anasema kwa sasa Kiwanda hicho kimeondoa changamoto hiyo ya ucheleweshwaji na sasa  mteja anapoagiza mahitaji yake ya samani ziwe kwa matumizi ya Ofisi au nyumbani mteja anapata mahitaji yake kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu hakuna tofauti tena ya ubora anaotengenezewa  na ule aliouona kwenye Maonyesho ya SabaSaba.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza John Itambu anasisitiza kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni ile ya bei za mbao kwa ajili ya kutengeneza samani zao kupatikana kwa shida kwa kuwa mafundi wengi wa mitaani hununua mbao kwa kutumia fedha taslimu na bila kupewa risiti za EFD sasa pale Jeshi la Magereza linapofuata taratibu za kupewa risiti za EFD  wauzaji wa mbao hutoa kipaumbele kwa mafundi wale wa uraiani wenye fedha taslimu badala ya Magereza, hivyo ni muhimu kwa Mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutumia mashine ama risiti za EFD.
‘‘Pamoja na kwamba mara nyingi wateja wanaona bei za bidhaa za kiwanda chetu cha samani ziko juu lakini wataalamu wetu wanachokiangalia ni kuzalisha bidhaa kwa kutumia mbao zenye ubora wa hali ya juu miti hasa ile ya asili, na ndio maana samani zetu zinadumu kwa muda mrefu huwezi kulinganisha ubora wake na bidhaa za mitaani’’ anasisitiza Mkuu wa Kiwanda hicho John Itambu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...