Na Benjamin Sawe

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2017 umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017. Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwezi Aprili, 2017.

“Mfumuko wa Bei wa Taifa umepungua kutoka asilimia 6.4 kwa mwezi Aprili, 2017 hadi kufikia asilimia 6.1 kwa mwezi Mei , 2017 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Mei, 2017,” amesema Kwesigabo. Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2017 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.2 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.5 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017.

Amesema Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 109.26 kwa mwezi Mei, 2017 kutoka 109.04 mwezi Aprili, 2017 kutokana na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Kwesigabo ametaja bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kuwa ni pamoja na mahindi yaliyoongezeka kwa asilimia 4.2, maharage mabichi kwa asilimia 2.9, maharage ya soya kwa asilimia 2.2, unga wa mtama kwa asilimia 1.5, viazi mviringo kwa asilimia 2.0, mihogo mikavu kwa asilimia 2.3, na magimbi kwa asilimia 2.5.

Aidha bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mkaa ulioongezeka kwa asilimia 2.5. Ameongeza kuwa Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Mei, 2017 umepungua hadi asilimia 11.8 kutoka asilimia 12.0 mwezi Aprili, 2017. Aidha, badiliko la Fahirisi za Bei kwa bidhaa zisizo za vyakula umepungua hadi asilimia 3.0 mwezi Mei, 2017 kutoka asilimia 3.4 mwezi Aprili, 2017.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo akiongea na wanahabari kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Mei 2017 jijini Dar es Salaam leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...