Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar           
Wananchi Zanzibar wameshauriwa kuchukua tahadhari kubwa zaidi wakati wa sherehe za Edd el Fitri katika kujikinga na maradhi ya kipindupindu ili kuhakikisha maradhi hayo hayaongezeki na kuleta athari zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi Mmoja, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohamed Abdallah ametaka tahadhari zaidi iwe ni kuwadhibiti watoto ili kuhakikisha hawali ovyo hasa katika kumbi na viwanja vya Sikukuu.
Aliwanasihi wananchi wasiwe tayari kukigeuza kipindi cha sikukuu kuwa cha madhara kwao na kuwashauri wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa wananchi wenzao kwa kuacha kufanya biashara za vyakula vilivyopikwa na juisi katika sehemu zisizoruhusiwa.
Alisema Wizara ya Afya imetoa mwongozo kuhusu biashara za vyakula vinavyoruhusiwa kuuzwa katika viwanja vya sikukuu ambazo ni bidhaa zilizotengenezwa viwandani.
Aidha alitaka familia ambazo zitapenda kuandaa chakula na kula nje ya nyumba zao katika sehemu za wazi kuhakikisha wanafuata masharti yote ya  afya ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kuanza kula.
Akizungumzia hali halisi ya kipindupindu Zanzibar tokea kilipoanza wiki tatu zilizopita, Dkt Fadhil alisema wagonjwa 303 wamelazwa katika kambi ya Chimbuni na Gamba iliyopo Wilaya Kaskazini A ambapo wanne kati yao wamefariki.
Alisema hivi sasa kambi ya Chumbuni imebakiwa na wagonjwa nane wa kipindupindu na kambi ya Gamba haina mgonjwa hata mmoja kuanzia tarehe 8 mwezi huu.
Alitaja sababu kubwa ya vifo hivyo vya watu wanne vilitokana na upungufu mkubwa wa maji mwilini na chanzo chake ni kucheleweshwa kupelekwa katika kituo cha afya.
 Dkt. Fadhil alikiri kuwa hali bado haijawa ya kutisha hadi hivi sasa lakini kumejitokeza ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu katika vijiji vya Bambi na Mpapa Wilaya ya Kati na wanafikiria kufungua kambi wakati wowote katika maeneo hayo iwapo hali  itaendelea kuwa hivyo.
Aliwasisitiza wananchi kuendelea kufuata masharti ya afya katika kupambana na Kipindupindu ikiwa ni pamoja na kuyatibu maji ama kuyachemsha kabla ya kunywa na kuhakikisha wanatumia vyoo na kukosha vizuri mboga za majani na matunda kabla ya kula.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...