THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

RAIS DKT. MAGUFULI AOMBOLEZA KIFO CHA MKURUGENZI MKUU WA AFDB KANDA YA AFRIKA KUSINI MAREHEMU DKT. TONIA KANDIERO


Dkt. Tonia Kandiero 

“Kwa mshituko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Kanda ya Afrika Kusini Dkt. Tonia Kandiero aliyefariki dunia ghafla jana usiku tarehe 28 Juni, 2017 akiwa ofisini kwake huko Pretoria Afrika Kusini”

Hii ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa leo tarehe 29 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kupokea taarifa za kifo cha Dkt. Tonia Kandiero ambaye kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka 2016 alikuwa Mwakilishi wa AfDB Tanzania.
“Nitamkumbuka Dkt. Tonia Kandiero kama mchapakazi hodari aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, nikiwa Waziri wa Ujenzi nimeshirikiana nae kwa karibu kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa nchi yetu ambayo imefadhiliwa na AfDB
"Ametoa mchango mkubwa kufanikisha ujenzi wa madaraja na barabara za Dodoma – Iringa, Dodoma – Babati, Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala, Arusha – Taveta – Voi na pia alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha miradi mingine ambayo ipo mbioni kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Tanga – Mombasa, Mbinga – Mbambabay na Tabora - Katavi”, amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kufuatia kifo cha Dkt. Tonia Kandiero Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa AfDB Dkt. Akinwumi Adesina, familia ya marehemu Dkt. Tonia Kandiero, wafanyakazi wote wa AfDB, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu.

Dkt. Magufuli amemuombea marehemu Dkt. Tonia Kandiero apumzishwe mahali pema peponi - Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Juni, 2017