Na Mwene Said wa Globu ya Jamii, Dar es Salaam.

Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu, jijini Dar es Salaam, imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, baada ya kutupilia mbali pingamizi la dhamana lililotolewa na upande wa Jamhuri.

Uamuzi huo ulitolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo. Alisema mahakama yake baada ya kupitia hoja za upande wa Jamhuri za pingamizi hilo haukuithibitishia mahakama kama kuna kesi kati ya hizo anazotuhumiwa aliwahi kuruka dhamana.

Alisema hoja ya mshtakiwa kuzuiwa dhamana kwa sababu ya usalama wake, haina mashiko na haijitoshelezi kuweza kumweka Lissu mahabusu.

Kuhusu jopo la mawakili 18 wa utetezi, hakimu alisema ni ishara wazi kwamba  inaonesha anaishi vizuri na watu na wanaupendo dhidi yake.

Hakimu alisema mashtakiwa atakuwa nje kwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaotoka serikalini au taasisi zinazotambulika, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 10 milioni kila mmoja.

Pia, alisema mshtakiwa asitoke nje ya jiji la  Dar es Salaam bila kibali cha mahakama hiyo. Lissu alitimiza masharti hayo na yuko nje kwa dhamana.

Wakili wa Serikali Simon Wankyo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika aliomba mahakama kupanga tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.

Hakimu Mashauri alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Agosti 24, mwaka huu.

Mapema Julai 24, mwaka huu Lissu alirudishwa rumande baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha pingamizi la dhamana kwa madai kuwa kwa maslahi ya usalama wake.

Hata hivyo, upande wa Utetezi uliongozwa na jopo la mawakili 18, akiwamo Fatuma Karume, Peter Kibatala, Samaa Salah, Dickson Matata, Faraji Mangula, Nashon Nkungu, Konda Johaness, Alex Masaba, Deus Mteja, Matojo Kosata, Novatus Muhangwa, John Mhozwa, Hassan Kihangyo, Jamhuri Johnson, Daim Halfan, Elisha Magabe (mke wa Lissu) na Boniface Mahela ulipinga pingamizi hilo.
Katika kesi ya msingi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa Julai 17, mwaka huu mtaa wa Ufipa uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno na lugha ya uchochezi dhidi ya Rais.

Alinukuu maneno hayo kuwa" Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini. Vibali vya kazi |(work permit) vinatolewa kwa wamishenari wa kikatoliki tu huku madhehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji.

Viongozi wakuu wa serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familima, kabila na ukanda...acheni woga pazeni sauti... kila mmoja wetu...tukawaambie wale ambao bado wanampa msaada wa pesa Magufuli na serikali yake kama tulivyowaambia wakati wa serikali ya makaburu, hii serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa isusiwe  kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi... yeye ni dikteta uchwara" mwisho wa kunukuu.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa maneno hayo ni ya uchochezi yenye lngo la kuvuruga amani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...