THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Nusu ya watanzania wanasema usalama umeimarika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita


 Kuna mtazamo wa jumla miongoni mwa wananchi kuwa usalama nchini umeimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kama inavyooneshwa na zaidi ya nusu ya wananchi hao (asilimia 53). Lakini asilimia 37 ya watanzania wanasema hali ya usalama imebaki vilevile huku asilimia 10 wanasema hali imekuwa mbaya zaidi.

Takwimu za Sauti za Wananchi za mwaka 2015 zilionesha kwamba asilimia 57 ya wananchi hawakuwahi kuhisi hawako salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi. Lakini mwaka 2017 idadi imeongezeka na kufikia asilimia 71. Kwa ujumla kwa mwaka uliopita, asilimia 29 ya wananchi hawakujisikia salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi au waliogopa kufanyiwa uhalifu kwenye nyumba zao (asilimia 26). Asilimia 16 walikiri kukaa majumbani mwao huku wakiwa na hofu ya uhalifu.
Pamoja na viashiria chanya kuhusu usalama, viwango vya uhalifu vinaonekana kuwa juu. Asilimia 41 ya wananchi wamewahi kushuhudia uhalifu ukifanyika hadharani ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Hapa usalama tu: Usalama, polisi na haki nchini Tanzania. Muhtasari huu unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simuza mkononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,805 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) mnamo mwezi Aprili mwaka 2017.


Vilevile takwimu hizi zinaonesha kwamba mara nyingi wananchi hawaombi msaada kwa polisi,hasa pale wanapokuwa wahanga wa uhalifu. Ni mwananchi mmoja tu kati ya wanne (asilimia 26) anayeomba msaada polisi. Hata hivyo, idadi hii inatofautiana kutokana na makundi mbalimbali: matajiri (asilimia 42) na wakazi wa mijini (asilimia 41) wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuomba msaada polisi. Wananchi wengine (asilimia 66), huenda kwanza kwa mwenyekiti wa kijiji/mtaa. Wakati huo huo, idadi kubwa ya wananchi imeripoti kutotoa kabisa taarifa za uhalifu: asilimia 21 wanasema hawatatoa taarifa za uhalifu zilizolenga kaya zao na asilimia 8 wanasema uhalifu kwenye jamii zao hautoripotiwa.
Bila shaka wananchi huamua kutotoa taarifa za uhalifu polisi kutokana na umbali wa vituo. Asilimia 27 ya wananchi hawana kituo cha polisi kwenye kata zao. Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo asilimia 50 wanasema hawana kituo cha polisi kwenye kata zao na asilimia 27 hutumia muda mrefu (zaidi ya dakika 30) kufika kwenye kituo cha polisi.