THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aomboleza kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa AFDB Kanda ya Afrika Kusini, Dk. Tonia Kandiero

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Benki ya Maendelea ya Afrika (AfDB) Dk. Akinwumi Adesina,kufutia kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Kanda ya Afrika Kusini, Dk. Tonia Kandiero,kilichotokea Juni 28, 2017 huko mjini Pretoria nchini Afrika Kusini.

Katika salamu hizo za rambi rambi, Dk. Shein alieleza kuwa ameshtushwa sana na kifo cha hafla cha Mkurugenzi huyo wa (AfDB) katika Kanda ya Afrika ya Kusini Dk. Tonia Kandiero ambacho kimeigusa sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na jamii mbali mbali za Bara la Afrika.


Dk. Shein alisema kuwa kwa niaba yake binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, wanatoa mkono wa pole kwa Rais Adesina, kwa Benki ya  AfDB, wafanyakazi wote wa Benki hiyo pamoja na ndugu na familia ya marehemu Tonia kutokana na msiba huo. 
Salamu hizo za Dk. Shein zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar pamoa na Serikali yao wanaendelea kumkumbuka marehemu kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuitembelea mara kwa mara kwa ajili ya kujumuika pamoja katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo katika sekta muhimu za kiuchumi na kijamii hasa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, elimu na miradi ya maji. 
“Daima tutaendelea kutoa shukrani zetu kwake kwa kurahisisha shughuli za uratibu na majadiliano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)  pamoja na wahusika wengine muhimu wa maendeleo kwani alikuwa mchapakazi mzuri na aliyetoa mchango mkubwa katika nchi hii” zilieleza salamu hizo za rambi rambi alizotuma DK. Shein. 
Aidha, salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa hikma zake, busara zake na mapenzi yake makubwa vyote kwa pamoja vitaendelea kukumbukwa sio kwa watu wa Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee bali zitakumbukwa na wapenda maendeleo wote duniani kutokana na mchango wake mkubwa. 
Sambamba na hayo, Dk. Shein katika salamu hizo za rambi rambi alimuomba Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk. Adesina,  kupokea salamu hizo kwa msiba huo mkubwa uliotokea na kumuhakikishia kuwa mawazo, fikra na majonzi ya Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla bado yataendelea katika kumkumbuka kiongozi huyo 
Dk. Shein alimuomba  Rais huyo wa (AfDB) kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa Wanafamilia, Wafanyakazi na viongozi wote wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). 
Pamoja na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema kiongozi huyo. 
Marehemu Dk. Tonia kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika ya Kusini mwishoni mwa mwaka 2016, alikuwa Mwakilishi wa Benki hiyo hapa nchini Tanzania ambaye alifanya kazi zake hapa nchini kwa takriban miaka sita. 

Na Mnamo Disemba 21 mwaka 2016 maremu Dk. Tonia, alifika Ikulu mjini Zanzibar kumuaga Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa anaelekea katika kituo chake kipya cha kazi huko Afrika ya Kusini, baada ya kupewa majukumu ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika Kanda ya Afrika ya Kusini.