WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia mwaka huu wa fedha, Serikali imepunguza gharama za malipo ya awali ya thamani ya ardhi iliyopimwa kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5.

“Serikali inaendelea kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi nchini na katika mwaka wa fedha 2017/2018, imepunguza tozo ya awali ya ardhi iliyopimwa (premium) kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa ardhi,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.

Amesema Serikali itahakikisha kuwa kila kipande cha ardhi ya Tanzania kinapimwa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. “Serikali imeweka mkakati na mpango kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya tano kila mwaka.”

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda kwa kupeleka wataalam wa kada mbalimbali na kuwawezesha kwa kuwapatia vitendea kazi stahiki. “Kazi ya upimaji wa ardhi haiwezi kufanikiwa bila ya rasilmali watu.Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za ardhi katika kanda badala ya kufuata huduma hizo makao makuu ya wizara,” amesema.

Amewasihi watumishi watakaohamishiwa katika ofisi za kanda pamoja na wale waliopo katika Halmashauri, wafanye kazi kwa ushirikiano na watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi na kutoa huduma kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...