THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

NGURUWE RUKSA KIBAHA BAADA YA KUPIGA MARUFUKU.

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani ,imesitisha zuio la kuingiza na kufanya biashara ya nguruwe na mazao yake ,:"ambapo juni mwaka huu ilipiga marufuku biashara hiyo ili kuepuka  na ugonjwa wa homa ya nguruwe(AFRICAN SWINE FEVER) .

Halmashauri hiyo ilichukua hatua hiyo kutokana na idara ya mifugo na uvuvi kubaini kuingia kwa ugonjwa huo katika baadhi ya maeneo .

Akizungumzia suala hilo ofisini kwake mjini humo,ofisa habari wa halmashauri ya mji wa Kibaha,Innocent Byarugaba,alisema  idara hiyo imefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa hakuna tena viashiria hivyo na kuamua kusitisha zuio hilo.

Aidha alieleza jumla ya nguruwe 71 wenye thamani ya sh.mil.4.970 walikufa kutokana na ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Kwa mujibu wa Byarugaba ,uwepo wa kuzuia na kusitisha kipindi hicho kulisaidia kupunguza na hatimae kudhibiti ongezeko na kuenea kwa ugonjwa huo .

"Halmashauri hii kuanzia sasa inapenda kuutarifu umma kuendelea na shughuli zake kama kawaida na kwamba zuio limeondolewa rasmi "alisema Byarugaba.
Alieleza sababu iliyosababisha kupigwa marufuku kuingia mnyama huyo na kuathiri hasa wauza kitimoto kwamba ni ugonjwa wa homa ya nguruwe kuingia kwenye kata mbili za Picha ya Ndege na Viziwaziwa eneo la Mikongeni. 

Nae Afisa mifugo na uvivu wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Charles Marwa ,alisema hatua za awali zilizochukuliwa ikiwemo kuzuia nguruwe kuingia na kutoka katika maeneo yaliyokuwa na viasharia.
"Sampuli mbalimbali za nguruwe waliokufa zilichukuliwa na kupelekwa maabara kuu ya mifugo Temeke Jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi na kubaini uwepo wa ugonjwa huo ,” alisema Marwa.

Marwa alibainisha ,ugonjwa wa African Swine Fever,ambao  unadaiwa kuingia  kwa nguruwe hauwezi kuambukiza binadamu ila madhara yake makubwa ni kuteketeza nguruwe wengi asilimia 100,kwa muda mfupi na kusababisha hasara kwa mfugaji.

Alitaja dalili za ugonjwa huo ni kuvuja na kusambaa kwa damu kwenye viungo vya mwili , homa kali, kupumua kwa shida na, kutapika.
Vifo ndani ya siku mbili hadi 10 na muonekano wa damu kuvilia kwenye viungo mbalimbali vya ndani vya nguruwe baada ya kumpasua.

Ugonjwa huo hushambulia nguruwe na hauna tiba kwa wanyama wanaoupata na husababisha vifo vingi unapotokea hasa kwa wanyama wakubwa.