Leo tarehe 2 Agosti, 2017, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yao nchini Vietnam, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba, wamekutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Vietnam, Mhe. NGUYEN XUAN PHUC, ambapo walijadili namna ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa kiuchumi na biashara baina ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya kukamilisha kongamano la tatu la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Vietnam lililofanyika siku hiyo hiyo ya tatu ya ziara yao.

Katika mazungumzo yao, Waziri Mkuu wa Vietnam aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua nzuri za kiuchumi inazoendelea kupiga kwa kuzingatia kwamba Tanzania ni kati ya nchi kumi duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na ni ya kwanza kwa Afrika Mashariki. Aliishukuru pia serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuisaidia kampuni ya Halotel katika utoaji wa huduma zake za mawasiliano na hasa vijijini. 
Aliwakikishia Mawaziri hao kuwa Vietnam itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha kuwa nchi hizo zinafikia malengo ya biashara yaliyowekwa na Marais wa nchi hizi hapo mwaka 2016 nchini Tanzania.

Kwa upande wake Waziri Mwijage alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua na kuenzi urafiki na ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili. Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuendeleza mikakati ya kutekeleza maelekezo ya viongozi wa nchi hizo mbili kwamba ifikapo mwaka 2020 biashara kati ya nchi hizi ifikie dola za marekanii bilioni 1. 


Hivyo, kongamano la uwekezaji lililofanyika hapo mjini Hanoi, limeweza kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania wapatao 30 na wafanyabiashara wa Vietnam zaidi ya 200. Aidha, kutokana na kongamano hilo, changamoto mbalimbali zilielezwa ambazo zinarudisha nyuma jitihada za wafanyabiasha. 
Alieleza kuwa tayari amekutana na Waziri wa Biashara na Biwanda wa Vietnam na wamekubaliana timu ya wataalmu ikutane Dar es Salaam mwezi Septemba kuanza kufanyia kazi mapungufu hayo kwa pande za nchi zote. Nae Waziri Dkt.  Tizeba alimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa nafasi aliyowapa ya kukutana pamoja na kuwa ana majukumu mengi. 

Alieleza kuwa changaoto nyingi zilizoelezwa na wafanyabiashara katika kongamano la biashara zingeweza kutatuliwa iwapo hati za makubaliano zilizopendekezwa na nchi hizo zingekuwa zimekamilishwa na kuwekwa saini. 
Hivyo, alimuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu asaidie kwa upande wa Serikali ya Vietnam ili hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi mbali mbali za Tanzania na Vietnam zikamilishe na kurahisisha biashara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...