Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi nchini. 

Lukuvi ametoa kauli hiyo wakati anazungumza na Globu ya jamii ambapo amefafanua kuna jitihada na mikakati mbalimbali inafanya kutatua migogoro ya ardhi. Amesema migogoro ambayo wizara yake inatafuta ufumbuzi mingi ni ile ya kuanzia mwaka 2015 kurudi nyuma kwani tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani hakuna mgogoro wa ardhi. 

"Kwa sehemu kubwa mimi na wasaidizi wangu tunakwenda vizuri katika kuhakikisha tunamaliza migogoro ya ardhi kama ambavyo dhamira ya Serikali hii inavyotaka. "Migogoro mingi imeshughulikiwa na hata iliyokuwepo ilitokana na kutoshughulikiwa kwa wakati.Baadhi ya watendaji hawakuwa  wakichukua hatua kwa haraka. 

"Kwa sasa wizarani wanajua nataka nini na ndio maana tunakwenda vizuri maana hatutaki kutumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi,"amesema Lukuvi. Ameongeza kwa kutambua namna ya utendaji kazi wa baadhi ya maofisa wake ndio maana anatumia mfumo wa kuita wananchi wenye matatizo ya ardhi na kisha kutafuta ufumbuzi wake tena hadharani. 

Waziri Lukuvi amesema kwa mwenendo wanaokwenda nao anaamini Serikali ya awamu ya tano itafika mahali hakutakuwa na migogoro mingi ya ardhi. Akizungumzia migogoro ya ardhi kwa Jiji la Dar es Salaam, Lukuvi amesema kwa siku tatu ambazo amekuwa akitatua migogoro ya ardhi kwa wale waliofika wizarani ameipatia ufumbuzi.

Amesema migogoro ya ardhi ambayo hajaishughulikia ni ile ambayo kesi zipo mahakamani kwani wizara yake haina uwezo wa kuingilia uamuzi wa mahakama. Alipoulizwa iwapo migogoro ya ardhi kwa Dar es Salaam ipo siku itakwisha, amejibu ana uhakika wa kuimaliza. 

"Kwa hali ilivyo itafika wakati hata tukiita watu wenye migogoro ya ardhi waje tuitatue hawatakuwepo maana tunakwenda vizuri katika kuishughulikia,"amesema.Amefafanua kwa sasa atakuwa na ratiba katika wilaya mbalimbali ambapo atakwenda kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam aliyefika katika wizara hiyo wakati anasikiliza wenye migogoro ya ardhi jana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...