Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa kampuni ya CHICO kutoka China, ili kuweza kuufungua mkoa wa Tabora na mikoa jirani ya katavi na kigoma.

Amesema hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati aliposimamishwa na wakazi wa kijiji cha Tura, wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, alipokuwa akikagua kambi ya mkandarasi na kuangalia hatua za awali za matayarisho ya ujenzi wa barabara hiyo.

Prof. Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 117.9 na utachukua miezi 24 mpaka kukamilika kwake."Serikali imeanza rasmi ujenzi wa barabara hii na sasa ni jukumu lenu kuhakikisha mnampa ushirikiano mkandarasi huyu ili mradi uwahi kukamilika mapema", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amefafanua kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu katika kukuza biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani. Ameongeza kuwa sasa Serikali imeshapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka daraja la Kikwete mpaka Uvinza, mkoani Kigoma na hivyo itasaidia wananchi wanaotumia usafiri wa mabasi kutoka mkoa wa Dar es Salaam mpaka mikoa ya katavi na Kigoma kupita kwenye lami njia nzima.
Mkandarasi kutoka kampuni ya CHICO kutoka China, Bw. li, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuhusu hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiwaonesha Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Queen Mlozi na Mbunge wa Jimbo la Igalula ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi, eneo ambapo ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami itajengwa, mkoani Tabora.
Tingatinga likikata miti kwa ajili ya kusafisha eneo ambapo ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami utaanza, mkoani Tabora. 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...