Na Veronica Simba – Mara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea na kukagua Mgodi wa Buhemba na ule wa CATA Mining Ltd iliyopo mkoani Mara ikiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.
Katika Mgodi wa Buhemba, Kamati ilielezwa kuwa, Serikali iliukabidhi Mgodi huo wa dhahabu kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2011 ili iuendeleze, kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Kampuni ya Meremeta Limited.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, aliieleza Kamati kuwa Shirika limekamilisha upembuzi yakinifu katika mabaki ya dhahabu yaliyoachwa kipindi cha nyuma ambapo umebaini kuwapo takribani tani 796,400 za mabaki ya mchanga wa dhahabu yenye wastani wa kilo 852 za dhahabu.
“Aidha, upembuzi huo ulibaini kuwa mabaki hayo ya mchanga yatachenjuliwa kwa kutumia teknolojia ya Carbon in Leach (CIL). Mtambo unatarajiwa kuchakata mabaki ya mchanga wa dhahabu kiasi cha tani 246,240 kwa mwaka,” alisema.
Aliongeza kuwa, tathmini ya kiuchumi ya mradi imeonesha gharama za uwekezaji zinakadiriwa kufikia Dola milioni 3.96 na kwamba gharama za uendeshaji kwa mwaka zinakadiriwa kufikia Dola milioni 4.46 na kutarajiwa kuingiza faida inayofikia Dola milioni 3.45 kwa mwaka.
Kuhusu tathmini ya mashapo katika miamba migumu, Kamati ilielezwa kuwa taarifa za kitaalam zinaonesha kwamba wakati Kampuni ya Meremeta inafunga uzalishaji katika mgodi, kiasi cha wakia 600,000 zilisalia kwenye miamba migumu.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa STAMICO imeamua kufanya upya tathmini ya mashapo hayo ili kujiridhisha. “Hadi sasa kiasi cha mashapo yenye wakia 441,772 kimethibitika kuwemo kwenye miamba migumu kutoka katika migodi ya wazi. Ukadiriaji wa mashapo unaendelea,” alisema.
Vilevile, ilielezwa kuwa Shirika lilifanikiwa kuchoronga shimo moja katika eneo la Nyasanero ili kutathmini mkanda mpya wa dhahabu. Tathmini kamili ya kiasi cha dhahabu kilichopo kwenye mwamba itakamilika mara baada ya kupokea majibu ya maabara.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia) akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, mambo kadhaa kuhusu Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mining uliopo Mara, walipotembelea Mgodi huo wakiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila (kushoto) wakishiriki katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, katika Mgodi wa CATA Mining mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.
 Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...