Na Munir Shemwea, Tabora
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Keyera amesema manispaa ya Tabora pekee inadai zaidi ya shilingi bilioni sita kwa wamiliki wa ardhi na mashamba mkoani humo kama kodi ya ardhi. 
Kayera alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji kata wa Manispaa ya Tabora alipokutana na watendaji hao kuhamasisha ulipaji wa kodi ya ardhi na mashamba katika mkoa huo, mkutano uliofanyika ukumbi wa VETA Tabora.
Alisema, mpaka kufikia sasa katika manispaa ya Tabora zimekusanywa jumla ya shilingi bilioni 3.2 ikiwa ni pungufu ya malengo waliyojiwekea ya kukusanya shilingi bilioni nne katika mwaka huu wa fedha unaoishia juni mwaka 2018.
Alisema, kanda yake inayohusisha mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Katavi imeanza kuchukua hatua kwa wadaiwa sugu wa kodi za ardhi kwa kuwapatia hati za madai ambapo wahusika watatakiwa kulipa madeni yao ndani ya wiki mbili na wasipofanya hivyo wanapelekwa mahakamani na huko vifaa vyao au nyumba zitauzwa kufidia deni huku umiliki nyumba ama shamba ukifutwa.
‘’Unapopelekwa mahakamani uwezekano wa kushinda haupo na pia itakulazimu kulipa gharama za madadlali kwa kushindwa kulipa’’ alisema Kamishana Msaidizi Kayera.
Kwa mujibu wa Kayera, kikao chake na watendaji wa kata za manispaa ya Tabora ni moja ya harakati za ofisi yake ya Kanda ya magharibi kuhakikisha kodi ya serikali inapatikana sambamba na kuwashirikisha watendaji kuwatambua na kuwapelekea hati za madai wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika mitaa yao ili kuwabana waweze kulipa madeni yao.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa ardhi Kanda ya Magharibi alisema, utaratibu wa kulipa kodi ya ardhi kwa sasa ni rahisi kwani unaweza kulipia kwa njia ya simu na malipo hayo yanafanywa na wananchi waliopimiwa maeneo yao ingawa serikali iko katika hatua za kuhakikisha maeneo yote ya mijini hata yale yasiyopimwa wamiliki wake wanalipa kodi ya ardhi.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera akizungumza na watendaji wa Kata za Manispaa ya Tabora jana wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya ardhi katika kanda hiyo mkoani Tabora, kampeni inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushoto ni Mwanasheria wa Kanda Ramadhani Jongo.

Watendaji wa Kata za Manispaa ya Tabora wakimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera (hayupo pichani) wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi katika kanda ya magharibi mkoani Tabora, kampeni inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mmoja wa watendaji wa kata  za Manispaa ya Tabora akichangia maoni wakati wa kampeni ya uhamasishaji wa kulipa kodi ya ardhi kanda ya magharibi ulioendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...