Na Rehema Isango, Arusha
Jumla ya kilomita 91 za mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya mkoani Mara zimeimarishwa na sasa timu za wataalam wa upimaji ardhi na ramani zimeanza kazi hiyo wilayani Ngorongoro katika mkoa wa Arusha.
Kiongozi wa timu ya wataalam kutoka Tanzania Bw. Isaack Marwa amefafanua kuwa jumla ya alama kuu 66 zenye umbile la pembetatu zimeimarishwa ambapo kati ya hizo, 47 zimejengwa upya baada ya kung’olewa na 19 zimekarabatiwa baada ya kuchakaa katika maeneo ya mbalimbali ya wilaya za Rorya na Tarime mkoani Mara. Amesema kuwa wamefanikiwa kuweka alama mpya ndogo  takriban 900 zenye umbile la pembe nne ambazo zinaonana na kwamba sasa zinawezesha eneo la lote la mpaka wa kimataifa mkoani Mara kuonekana kwa urahisi ambapo kazi hiyo imetumia muda wa mwezi moja na majuma mawili.
Pamoja na kazi ya uwekaji wa alama, pia kazi ya usafishaji wa eneo la mpaka kwa urefu wa mita tano kwa kila upande wa nchi imefanyika  kwa kufyeka miti na kuwezesha alama hizo kuonekana kwa urahisi zaidi. Bw. Marwa amesema kuwa hivi sasa wameanza kazi mkoani Arusha baada ya kuruka kwa muda eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara lenye urefu wa kilomita 51 kutokana na mvua kuharibu barabara zinazotakiwa kufikisha vifaa vya ujenzi wa alama pamoja na wataalam.   
“Tumelazimika kuendelea na kazi hii katika kijiji cha Ololosokwan kilichopo katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha ambacho kimepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kisha  tutarejea nyuma kumalizia kipande tulichokiruka baada ya njia zinazotusaidia kufikisha vifaa na wataalam hifadhini kuimarika.” Alisema Bw. Marwa
Alisema kuwa tayari kilomita 21 zimefanyiwa kazi mkoani Arusha kwa hatua za awali kwa kuwa kazi hii hufanyika kwa mpangilio wa timu zilizoundwa kitaalam hadi kufikia uwekaji wa alama za mpaka. Kazi ya uimarishaji wa mpaka kati ya Tanzania na Kenya inayolenga kuwezesha Serikali   kusimamia kwa ufanisi shughuli za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama  ilianza katikati ya Mwezi Machi mwaka huu ambapo Kilomita 238 zinaimarishwa kutoka kando ya Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.  
 Bw. Nairoti Kenanda kutoka kijiji cha Njoroi katika tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha akishiriki kuchimba shimo lenye urefu wa mita moja kwa ajili ya kuwekwa alama ndogo ya mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya unaopita katika kijiji hiko.
Wanakijiji wa Kijiji cha Sukenya katika kata ya Soitsambu wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakisoma vipeperushi walivyopewa wakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kuhusu uimarishaji wa mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya ulioanza mkoani Arusha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...