Wakazi wa kata ya Kiruru iliyopo wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameanza kupata maji safi na salama kwa matumizi mbalimbali ,kutokana na kuzinduliwa kwa mradi wa maji katika eneo lao. 

Mradi huo ambao una uwezo wa kuhudumia kaya 427 zenye wakazi zaidi ya 2,135 umejengwa na shirika la Water Mission Tanzania, wakishirikiana na shirika la Rotary Club ya Mwanga, Rotary International na Rotary Foundation. Kata ya Kiruru inayojumuisha vijiji vya Heria, Msikitini, Bhughuru na Mighareni, kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na tatizo la maji safi kutokana na kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya maji kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo. 

 Mkuu wa wilaya ya Mwanga,Bw. Aron Mbogho, ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo alisema “Leo ni siku ya kihistoria kwa wakazi wa kata ya Kiruru, kutokana na kuanzishwa kwa mradi huu mpya wa maji safi na salama katika eneo hili,ambao utawahakikishia wananchi kupata maji safi na salama wakati wote. 

Kwa niaba ya serikali napenda kutoa shukrani kwa shirika la Water Mission Tanzania na Washirika wake kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kukabiliana na changamoto ya tatizo la maji safi na salama kwenye jamii mbalimbali” Bw. Mbogho, alisema mradi huu utanufaisha wakazi wote wa kata ya Kiruru, hususani Wanawake ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji safi kwa ajili ya matumizi ya familia zao. Aliwataka wananchi wa Kiruru kutoa ushirikiano kwa wadau waliofanikisha mradi huu sambamba na kutunza miundombinu ya mradi ili uweze kuwa endelevu. 

“Kuwepo mradi huu katika eneo hili kutapunguza kwa kiasi kikubwa maradhi mbalimbali yatokanayo na matumizi ya maji yasio salama” alisisitiza. Mratibu wa Huduma za Maendeleo wa Shirika la Water Mission Tanzania, Isack Abdiel alisema “Tunayo furaha kubwa siku ya leo kutokana na kukamilisha mradi huu mpya hapa wilayani Mwanga ambao unazinduliwa leo. Mradi huu ni mwendelezo wa jitihada za shirika letu kuunga mkono jitihada za serikali za kukabiliana na changamoto ya kumaliza tatizo la maji kwenye jamii. Nina imani wakazi wa eneo hili la mradi mtahakikisha mnatunza miundombinu ya mradi ili uwe endelevu kwa matumizi ya sasa na ya vizazi vijavyo”.

 Isack Abdiel pia alishukuru viongozi wa serikali wa wilaya ya Mwanga na wadau wengine kwa kuunga mkono Shirika la Water Mission Tanzania, na kwa kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa mradi huu hadi kufikia sasa ambapo umefikia hatua ya kuzinduliwa. Shirika la Water Mission Tanzania, lilianza kufanya kazi nchini Tanzania, mnamo mwaka 2013 likiwa linajishughulisha na ujenzi wa miradi ya kukabiliana na changamoto ya maji kwenye jamii. Hadi sasa Shirika lina miradi katika mikoa zaidi ya 6 ikiwemo, Dodoma, Arusha, Geita, Kagera, Kigoma and Tanga na Kilimanjaro. 

 Ofisi za makao makuu ya shirika hili kwa hapa nchini yapo jijini Dar es Salaam ambayo inaratibu miradi yote inayoendeshwa na shirika hapa nchini. Mbali na Tanzania shirika la Water Missions International, linaendesha miradi ya kukabiliana na changamoto ya maji katika nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Haiti, Honduras, Mexico, Peru, Belize na Indonesia.
Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Bw. Aron Mbogho akikata utepe kuzindua mradi.
Mmoja wa wakazi wa kata ya Kiruru akitwishwa ndoo ya maji aliyochota kwenye mradi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wakifuatilia matukio.
Afisa mwandamizi wa Water Mission Tanzania,Isack Abdiel akiongea wakati wa hafla hiyo --- 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...