Timu ya soka ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imetwaa kombe la benki ya Standard Chartered baada ya kuitandika kwa mikwaju ya penalti  2-1 timu ya Mwananchi Communications Limited .

Kwa ushindi huo, timu ya TBL sasa itakuwa na ziara ya siku 3 nchini Uingereza na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya Standard Chartered yaliyopangwa kufanyika kwenye uwanja wa Anfield, Septemba mwaka huu.Aidha timu hiyo ya TBL wakifika Anfield wataona mechi ya msimu mpya wa EPL mubashara na kuzungumza na magwiji na kupata nafasi ya kunolewa nao.

Katika michuano hiyo Mchezaji wa Mwananchi, Saidi Seif alifunga mabao manane na kuwa mfungaji bora.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na gwiji la timu ya Liverpool, Sami Hyypia walishuhudia mechi hiyo na kutoa zawadi kwa washindi.

Akizungumza mara baada ya mashindano hayo kumalizika, Dk Mwakyembe aliipongeza timu ya TBL kwa kutwaa ubingwa na kuishukuru benki ya Standard Chartered kwa kutoa mchango wake kukuza sekta ya michezo.
“Naipongeza benki ya Standard Chartered kwa kuendesha mashindano haya na kuleta hamasa katika soka, nimefarijika sana na nimeshuhudia vipaji vingi, soka ina wigo mpana na ninaamini tunaweza kufanya vyema katika mashindano mbalimbali kwa kutumia vipaji vyetu,” alisema Dk Mwakyembe.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Sanjay Rughani alisema kuwa benki yao ni wadau wakubwa wa maendeleo ya michezo nchini na katika sekta nyingine na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kwa maendeleo ya taifa.
 Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Sanjay Rughani kwa pamoja wakikabidhi kombe kwa kapteni wa kampuni ya TBL mara baada ya kutwaa ubingwa wakombe la benki ya Standard Chartered baada ya kuitandika kwa mikwaju ya penalti  2-1 timu ya Mwananchi Communications Limited katika mashindano yaliyofanyika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
 Mabingwa wa mashindano ya kombe la benki ya Standard Chartered kampuni ya Bia ya TBL wakishangilia mara baada ya kukabidhiwa kombe hilo wakati mashindano hayo yalipofikia tamati mwishoni wa wiki katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (kulia) akimpongeza Gwiji la soka, klabu ya Liverpool, Sami Hyypia (wa pili kushoto) kwa kuja nchini kushuhudia mashindano ya kombe la benki ya Standard Chartered yaliyofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Sanjay Rughani (wa pili kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi (kushoto).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...