Na Jumia Travel Tanzania

Msimu wa majira ya joto au ‘Summer Season’ kama unavyojulikana kwa nchi za Ulaya na Marekani huwa ni kipindi cha mapumziko miongoni mwa watu wengi. Mapumziko haya si hufanywa tu na watu wa kawaida kutokea nchi hizo bali pia watu mashuhuri kama vile wacheza soka, wanamuziki, wafanyabiashara na wanasiasa.

Sababu kubwa zinazopelekea watu wa mataifa hayo kuchukua muda wa likizo ni kutokana na kipindi hiki kuwa na hali ya hewa nzuri. Kipindi kirefu cha mwaka kwenye maeneo yao hutawaliwa na baridi kali pamoja na barafu katika maeneo mengi.

Matokeo ya hali hii ni nchi tofauti zenye vivutio vya kitalii kunufaika kwa kiasi kikubwa kwani hupokea maelfu ya watalii. Miongoni mwa sehemu zinazotembelewa kwa kiasi kikubwa ni pamoja na Afrika, Tanzania ikiwemo.
Kwa mfano hivi karibuni tumeshuhudia watu mashuhuri kama vile Rais aliyepita wa Marekani, Barack Obama na familia yake wakitembelea Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti kwa muda wa takribani wiki nzima. Naye, Rais wa sasa wa nchi ya Uswizi, Mh. Alain Berset aliyeingia Tanzania na kutarajiwa kutumia siku 15 kutalii vivutio kadhaa kama vile Serengeti, Tarangire, Manyara, Ngorongoro na Zanzibar. 

Pia tumeshuhudia mchezaji wa timu ya Taifa ya Hispania na klabu ya Atletico Madrid, Koke akiwa amekuja kupumzika na familia yake katika mbuga ya Serengeti mara baada ya timu yake kuondolewa katika michuano ya Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zinazohusu masuala ya utalii, visiwa vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, mbuga ya Serengeti na hifadhi ya bonde la Ngorongoro ni miongoni mwa vivutio vilivyopo kwenye orodha ya watalii wengi duniani.
Akizungumzia juu ya sababu zinazopelekea kukua kwa utalii wa ndani ya nchi pamoja na bara la Afrika, Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Travel Tanzania, Bw. Kijanga Geofrey amebainisha kuwa kujitangaza ndani na kimataifa, gharama nafuu za malazi na usafiri pamoja na uboreshwaji wa miundo mbinu ya usafiri ni vichocheo vikubwa.

“Tumeshuhudia taasisi zilizopewa mamlaka na serikali zikishiriki maonyesho ya kimataifa ya utalii ndani na nje ya nchi. Hii hutoa fursa kwa watalii na wadau wa sekta kujua vivutio vilivyopo na taratibu za kuvitembelea. Lakini maboresho katika sekta za usafiri hususani wa anga ambao ndio hutumiwa na asilimia kubwa ya watalii duniani umeleta chachu nchini,” alisema Bw. Geofrey.

Tanzania imekuwa ni kitovu cha utalii wa ndani ya Afrika ambapo hupokea watalii wengi kutokea nchi za Afrika ya Kusini, Nigeria na Kenya. Nchi hizi ambazo zina idadi kubwa ya watu barani Afrika na uchumi mzuri ni fursa kubwa ya kimasoko endapo zitatumiwa vizuri kutangaza vivutio vilivyopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...