Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Penny Mordaunt ametangaza msaada huo Ijumaa tarehe 10 Agosti, 2018 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Mordaunt amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Mhe. Rais Magufuli ambapo kati yake shilingi Bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususan kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi Bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na shilingi Bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Mhe. Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo” amesema Mhe. Penny Mordaunt.

Ameongeza kuwa pamoja na kuwa wachangiaji wakubwa katika bajeti ya Serikali, Uingereza ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na kwamba wanafurahishwa na wito wa Mhe. Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kutoka Uingereza watakaowekeza kwa manufaa ya pande zote (win-win).

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amemuahidi Mhe. Penny Mordaunt kuwa fedha zilizotolewa kiasi cha shilingi Bilioni 307.5 zitatumika vizuri na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha uhusiano wa Tanzania na Uingereza unazidi kuimarishwa kwa kuwa inatambua kuwa Uingereza ndio mwekezaji mkubwa hapa nchini na imekuwa ikitoa misaada mikubwa ya fedha za walipa kodi wa Uingereza kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

Pia, Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Mhe. Penny Mordaunt albamu ya picha za shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika vibaya kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016, na ameishukuru Uingereza kwa msaada wa shilingi Bilioni 6 zilizotumika kujenga majengo hayo kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye amesema ziara ya Waziri Penny Mordaunt imezidi kukuza uhusiano wa Tanzania na Uingereza.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Agosti, 2018
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam Ijumaa Agosti 10, 2018.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuonesha albamu ya picha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt inayoonesha Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa kabisa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera lililotokea Septemba 10, 2016  ambayo imejengwa upya na serikali ya Uingereza kupitia mpango wake wa maendelo ya elimu kupitia UKAid/DFID. Picha hizo zinaonesha shule hiyo baada ya tetemeko, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi siku ya mwaka mpya wa 2017 na inavyoonekana sasa baada ya kujengwa upya. Mhe. Mordaunt, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi, alimtembelea  Rais Dkt. Magufuli akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam Ijumaa Agosti 10, 2018.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpa zawadi ya kinyago cha "Umoja"  Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke (kulia), na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy (kushoto) Ikulu jijini Dar es salaam Ijumaa Agosti 10, 2018.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mikono na na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke aliyeongozana na , Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana pia na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy aliyeongozana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke,  walipomtembelea  Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018  Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wanahabari na kuishukuru serikali ya Uingereza  kwa misaada yake mbalimbali ikiwemo Shilingi Bilioni 307.5  kwa kuunga mkono juhudi zake za kupambana na rushwa pamoja na kuboresha sekta za afya na elimu baada ya kukutana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018.
Picha na IKULU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...